
BUDAPEST, HUNGARY. Wanasema sukuma presha, shambulia upande wa kushoto na linda kama maisha yako hatarini. Arsenal wapo hatua moja kutoka kuandika historia usiku wa leo.
Kushinda fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya leo mjini Budapest kutamfanya kocha Mikel Arteta na timu yake kuwa mashujaa wa kihistoria.
Watakuwa mabingwa wa 25 tofauti wa mashindano hayo (ikijumuishwa na enzi za Kombe la Ulaya), na baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England iliyopita watakuwa klabu ya nne ya Kiingereza kuwa na mataji mawili Ulaya ndani ya msimu mmoja. Historia inawasubiri. Iko mikononi mwa Arsenal. Wako umbali wa dakika 90 tu.
Tatizo pekee ni kwamba Paris Saint-Germain ndiyo wanaoweza kuwazuia. Hiyo ina maana Arsenal wanapaswa kuwashinda mabingwa watetezi wa Ulaya ili kuchukua taji au kucheza kwa dakika 120 na kutumaini watashinda kwa penalti.
PSG ilishinda fainali ya msimu uliopita dhidi ya Inter Milan kwa mabao 5-0, baada ya kuziondoa Liverpool, Aston Villa na Arsenal, na msimu huu wameziangusha Monaco, Chelsea, Liverpool na Bayern Munich kwenye hatua za mtoano.
Wana rekodi bora dhidi ya klabu za Ligi Kuu England wakishinda kila moja ya mechi zao tano za mwisho dhidi ya wapinzani wa Kiingereza.
Kwa kuwaondoa Bayern Munich ambao waliwafanya waonekane wamesimama mbali katika mechi ya marudiano, walithibitisha wanaweza kumshinda yeyote.
Mabingwa wa Ujerumani wakati huo walikuwa timu bora zaidi duniani kwenye viwango vya taasisi mbalimbali za uchambuzi wa soka.
Nafasi ya kwanza sasa inashikiliwa na Arsenal waliopanda hadi kileleni wiki iliyopita, na hakuna shaka kuwa ni tishio kubwa kwa matumaini ya PSG ya kutetea ubingwa wao.
Lakini kama Arsenal wanataka kuwangoa mabingwa watetezi, watahitaji kucheza kwa kujitoa bila ya kuacha kazi ya ulinzi kwa mabeki pekee kufanya kazi ya ziada kuzima safu ya ushambuliaji ya PSG iliyojaa vipaji.
Iwapo Arsenal watashinda, wengi wangetarajia ushindi mdogo na huenda wakamaliza mechi bila kuruhusu bao. Hakuna timu katika ligi tano bora za Ulaya iliyoshinda mechi nyingi zaidi msimu huu kwa ushindi wa bao 1-0 kama Arsenal (11).
Hata hivyo, licha ya uimara wa ulinzi wa Arsenal, kuwazuia Ousmane Dembele, Desire Doue na Khvicha Kvaratskhelia ni changamoto ambayo ni wachache huweza kuhimili.
PSG wanahitaji bao moja zaidi katika Ligi ya Mabingwa kufikia rekodi ya Barcelona ya mabao 45 kwa msimu mmoja (1999-00).
Kwa ujumla, wamefunga angalau bao moja katika mechi 27 za mwisho, wakifunga jumla ya mabao 62 ikiwa ni wastani wa mabao 2.24 kwa kila mechi.
Wapinzani wengi katika mfululizo huo wako chini ya kiwango cha Arsenal, lakini hivi karibuni PSG walifunga mabao manne dhidi ya Liverpool katika mechi mbili, matano na kisha matatu dhidi ya Chelsea, na matano dhidi ya Bayern.
Huenda mkakati wa msingi wa Inter Milan katika fainali ya msimu uliopita ulikuwa kujilinda kwa muda mrefu kadiri iwezekanavyo, na matokeo yake yalionekana.
Jumamosi hii, Arsenal huenda wakalazimika kudhani PSG watafunga bao wakati fulani, hivyo huenda wakahitaji kushambulia zaidi.
Huenda hilo lisishangaze sana ukizingatia walivyocheza dhidi ya Manchester City mwezi uliopita kwenye Uwanja wa Etihad. Siku hiyo, Arsenal walicheza kwa presha kubwa kuanzia mwanzo wakifanya mashinikizo 474, zaidi kuliko mechi nyingine yoyote ya Ligi Kuu England msimu huu. Hawakurudi nyuma wakati wowote, na kazi ya Kai Havertz katika kuweka shinikizo juu ilisababisha bao lao pekee.
PSG wana tabia ya kufanya makosa. Mabingwa hao wa Ulaya wamefanya makosa mengi yaliyosababisha mpinzani kupiga mashuti mengi (26) katika Ligi ya Mabingwa msimu huu, na pia makosa mengi yaliyochangia mabao sita.
Takwimu hizo zinaathiriwa na PSG kucheza mechi nyingi zaidi, lakini hata kwa wastani wa kila mechi, hawapo vizuri sana; nafasi ya nne kwa makosa yanayosababisha shuti na nafasi ya tisa kwa makosa yanayochangia bao.
Wanapata shida kucheza kuanzia nyuma licha ya ubora wao wa kiufundi. Ni timu mbili tu ambazo zimepoteza mpira karibu na lango lao zaidi kuliko PSG (mara 141), wastani wa mara 8.8 kwa kila mechi.
Muhimu zaidi ni kwamba, ni timu mbili tu zimefungwa mabao mengi zaidi baada ya kupoteza mpira wakiwa juu uwanjani kuliko PSG (4), na ni timu sita tu zilizo na wastani mbaya zaidi (0.25 kwa mechi).
Tottenham Hotspur walifunga bao baada ya kupora mpira juu ya uwanja katika kichapo cha mabao 5-3 huko Paris, na pia walifunga kutokana na kona, jambo ambalo Arsenal wanaweza kuliangalia kama fursa ya kumaliza mechi.
Umahiri wa Arsenal katika mipira ya adhabu (set-pieces) unajulikana, na ingawa si udhaifu mkubwa kwa PSG, hauwezi kuwa pekee unaoweza kusaidia.
Ni timu tano tu za Ligue 1 zilizo na asilimia kubwa ya mabao kutokana na mipira ya adhabu (20.7%), na hawajawahi kukutana na tishio kama la Arsenal.
Hata hivyo, mipira ya adhabu ni michache, na Arsenal hawawezi kutegemea sana hilo, hivyo huenda wakalenga zaidi upande mmoja ambapo PSG wanaonekana kuwa na udhaifu ambao ni wa kulia.
Kwa Achraf Hakimi, PSG wana beki wa kulia anayeshambulia sana duniani, na anasonga mbele kila nafasi inapopatikana. Lakini hilo linaacha nafasi nyuma.
Kati ya timu 36 za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu ni PSV na Chelsea pekee zilizotengeneza nafasi nyingi zaidi upande wa kulia dhidi ya PSG (37.3%). Spurs na Chelsea walifunga kupitia mashambulizi ya upande huo, huku bao la Luis Diaz wa Bayern likitokana na mbio za kuvunja safu ya ulinzi ambapo Hakimi hakumfuatilia.
Upande wa kushoto wa Arsenal ndio sehemu yenye sintofahamu kuelekea mechi ya leo, Jumamosi. Leandro Trossard amecheza mara nyingi, lakini kuna hoja kwamba kasi na uelekeo wa Gabriel Martinelli unaweza kuwa muhimu zaidi dhidi ya nafasi nyuma ya mabeki wa PSG.