Moshi. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Morogoro, imethibitisha hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa Ramadhani Yahaya maarufu Msabaha, aliyokuwa amehukumiwa baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka bibi wa miaka 64.

Awali, katika kesi ya jinai namba 17597/2025 Mahakama ya Wilaya ya Kilosa ilimtia hatiani kwa makosa mawili ambapo kosa la kwanza la ubakaji alihukumiwa kifungo cha miaka 30 na miaka miwili kwa shambulio lililosababisha madhara, adhabu ziizoenda kwa pamoja.

Hukumu iliyothibitisha adhabu hiyo imetolewa Mei 29, 2026 na Jaji Stephen Magoiga aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo ya jinai namba 2346/2026 iliyokuwa imekatwa na Ramadhani.

Jaji Magoiga, amesema Mahakama imebaini ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ulikuwa wa kuaminika, thabiti na uliothibitishwa na ushahidi wa kitabibu kiasi cha kuondoa shaka yoyote kuhusu hatia ya mrufani.

Ilivyokuwa

Awali ilidaiwa tukio hilo lilitokea Juni 17, 2025 katika kitongoji cha Mji Mwema, Kata ya Kimamba wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, ambapo Ramadhani alimbaka bibi huyo.

Ilidaiwa katika tarehe hiyo na eneo hilohilo, Ramadhani alimshambulia mwathirika wa tukio hilo kinyume cha sheria kwa kumkata vidole viwili vya mkono wa kulia kwa kutumia sime.

Mwathirika wa tukio hilo ambaye ni mmoja wa mashahidi wa jamhuri aliiambia mahakama kuwa Ramadhani alimtishia kwa sime na kumjeruhi kwa kumkata vidole viwil  muda mfupi baada ya kumbaka.

Alidai baada ya hapo Ramadhani alikimbia eneo la tukio, ambapo yeye alipiga kelele kwa jirani yake aliyeongozana naye hadi Kituo cha Poisi kisha hospitali ambapo alichunguzwa na kutibiwa.

Katika utetezi wake Ramadhani alidai siku hiyo wakiwa shambani bibi huyo alijeruhiwa vidole vyake vinne kisha wakarudi nyumbani na kuwa mwathirika wa tukio hilo (bibi huyo) alikuwa mpenzi wake.

Alidai walipofika nyumbani walifanya tendo la ndoa kisha asubuhi akaondoka na akiwa njiani alisikia kuna mtu ameiba mabati ambapo alikamatwa na kubambikizwa kesi hiyo baada ya kukataa kumtaja aliyehusika na tukio hilo.

Baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama ya Wilaya, Ramadhani alikata rufaa akiwa na sababu nne hiyo kwa misingi minne ikiwemo Mahakama ya mwanzo ilimtegemea udhaifu wa utetezi wake kumtia hatiani, iliamini ushahidi usioaminika wa mlalamikaji na kushindwa kutathmini ipasavyo ushahidi wa upande wake.

Aidha, alidai kuwa kesi hiyo haikuthibitishwa kwa kiwango cha kutosha cha kisheria na kwamba ngono iliyofanyika kati yake na mwathiriwa ilikuwa ya hiari kwa kuwa walikuwa katika uhusiano wa kimapenzi.

Upande wa mjibu rufaa (Jamhuri) ulipinga rufaa hiyo ukieleza kuwa kesi hiyo ilithibitishwa pasipo kuacha shaka na kuomba Mahakama itupilie mbali rufaa hiyo na kuthibitisha hukumu hiyo.

Uamuzi Mahakama

Jaji Magoiga amesema amezingatia kwa makini rekodi ya rufaa,ushahidi ulivyorekodiwa,mawasilisho ya pande zote na kwa kuwa hiyo ni rufaa ya kwanza, Mahakama hiyo ina wajibu wa kutathmini upya ushahidi wote na kufikia hitimisho.

Amesema baada ya kupitia upya ushahidi wote uliotolewa katika mahakama ya mwanzo, alijiridhisha kuwa hukumu ya awali ilitokana na nguvu ya ushahidi wa upande wa mashtaka na si udhaifu wa utetezi wa mrufani kama alivyodai.

Mahakama ilibainisha kuwa mwathiriwa alitoa maelezo ya kina kuhusu namna alivyotishiwa kwa sime, kushambuliwa na kisha kubakwa na mrufani.

Jaji amesema ushahidi huo uliungwa mkono na ripoti ya daktari iliyowasilishwa mahakamani kupitia fomu ya polisi namba tatu (PF3).

Amesema kwa mujibu wa ushahidi wa kitabibu, mwathiriwa alikutwa na michubuko pamoja na wekundu katika sehemu zake za siri, hali iliyoonesha kuwepo kwa kupenya kwa nguvu na kuwa daktari aliyemchunguza alithibitisha kuwa majeraha hayo yalikuwa yanaendana na tukio la ubakaji.

Mahakama pia ilizingatia ushahidi wa jirani wa mwathiriwa ambaye alisikia kelele za kuomba msaada na alipofika eneo la tukio alimwona mrufani akikimbia akiwa ameshika sime.

Jaji Magoiga amesema ushahidi huo uliimarisha simulizi ya mwathiriwa na kuondoa uwezekano wa kutungwa kwa kesi dhidi ya mrufani.

Kuhusu hoja ya kwamba mwathiriwa alikuwa mpenzi wa mrufani, mahakama ilisema hata kama madai hayo yangekuwa ya kweli, bado sheria inahitaji ridhaa ya mhusika wakati wa tendo husika.

Mahakama ilisema majeraha yaliyopatikana kwenye vidole vya mwathiriwa yalionesha wazi kuwa kulikuwa na mapambano na upinzani dhidi ya kitendo hicho, jambo lililothibitisha kutokuwepo kwa ridhaa.

Aidha, Jaji alibainisha kuwa mrufani mwenyewe hakukanusha kufanya ngono na mwathiriwa, bali alisisitiza kuwa ilikuwa ya hiari. Hata hivyo, ushahidi wa kitabibu pamoja na mazingira ya tukio ulionesha kuwa tendo hilo halikufanyika kwa makubaliano.

Katika uchambuzi wake, Jaji Magoiga alinukuu maamuzi mbalimbali ya Mahakama ya Rufani yaliyowahi kueleza kuwa ushahidi wa mwathiriwa katika kesi za ubakaji unaweza kutosha kuthibitisha kosa hilo ikiwa utaonekana kuwa wa kuaminika na kuungwa mkono na ushahidi mwingine.

Mahakama ilisema ushahidi wa mwathiriwa katika shauri hilo ulikuwa wa moja kwa moja, wa kuaminika na ulioungwa mkono na ushahidi wa kitabibu pamoja na ushahidi wa shahidi aliyefika eneo la tukio mara baada ya kusikia mayowe.

Kwa upande wa kosa la shambulio, mahakama ilikubaliana na hitimisho la mahakama ya mwanzo kwamba majeraha yaliyopatikana kwenye vidole vya mwathiriwa yalitokana na kukatwa kwa kitu chenye ncha kali, hali iliyolingana na maelezo kwamba alijeruhiwa kwa sime wakati akijaribu kujinusuru.

Baada ya kuchambua misingi yote minne ya rufaa, Mahakama Kuu ilihitimisha kuwa hakuna hata msingi mmoja uliokuwa na uzito wa kubatilisha hukumu ya awali.

“Upande wa mashtaka ulithibitisha makosa yaliyoshtakiwa bila shaka yoyote. Mahakama ya mwanzo ilitathmini ipasavyo ushahidi wa upande wa mashtaka na wa utetezi kabla ya kufikia uamuzi wake,” imeeleza sehemu ya hukumu hiyo

 Mahakama Kuu ilitupilia mbali rufaa yote na kuthibitisha hatia pamoja na adhabu zilizotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Kilosa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *