MOSHI: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Watanzania kutokubali kuwakabidhi watu wasio na sifa na uzoefu wa uongozi dhamana ya kuongoza nchi, kikisisitiza kuwa uongozi wa taifa si jambo la majaribio bali unahitaji viongozi wenye maono, uzoefu na uelewa wa mahitaji ya wananchi.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi ameyasema hayo Mei 30, 2026 alipotembelea na kushiriki kikao katika Shina Namba Mbili, Tawi la Bohora, Kata ya Njoro, Wilaya ya Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza baada ya kusomewa taarifa fupi ya kikao hicho, Kihongosi amesema CCM imekuwa ikiongoza taifa kwa miongo mingi na imejijengea uzoefu mkubwa katika kusimamia maendeleo, kulinda amani na kudumisha umoja wa Watanzania.

“Kwa msingi huo msiwakabidhi watu wasio na leseni ya kuongoza nchi. Uongozi wa taifa si jambo la majaribio, taifa linahitaji watu wenye uzoefu, wenye maono na wanaoelewa historia, changamoto na mahitaji ya wananchi wake,” amesema Kihongosi.

Amesema Mkoa wa Kilimanjaro una historia kubwa katika uongozi wa nchi kutokana na kutoa viongozi wengi mashuhuri waliolitumikia taifa kwa nyakati tofauti, hivyo wananchi wake wana wajibu wa kuendeleza misingi bora iliyoasisiwa na watangulizi wao.

Kihongosi amesisitiza umuhimu wa ushirikiano, mshikamano na kuendelea kuwaamini viongozi wanaotambua wajibu wao wa kuiongoza nchi mbele, huku akiwataka Watanzania kuendelea kulinda tunu za amani, umoja na mshikamano ambazo ni msingi wa maendeleo ya taifa.

Wakati huo huo, Kihongosi ametembelea na kuzindua Shina la Wakereketwa wa Manyema Relini, Kata ya Bondeni wilayani humo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukagua na kuimarisha uhai wa chama kuanzia ngazi ya msingi.

Akisoma taarifa fupi ya uzinduzi wa shina hilo, Katibu wa Shina la Wakereketwa, Habibu Rashid amesema wanatarajia kuongeza idadi ya wanachama na kuimarisha shughuli za chama katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *