
Winga Anthony Gordon (25) ameishukuru Newcastle United kwa mchango mkubwa ambao imekuwa nayo katika maendeleo yake muda mfupi baada ya kujiunga na Barcelona.
Jana Ijumaa, Mei 29, 2026, Gordon ametambulishwa rasmi na Barcelona kwa uhamisho ambao umegharimu kiasi cha Pauni 70 milioni (Sh247 bilioni) akitokea Newcastle United.
“Nimefurahia kila dakika niliyocheza Newcastle. Kuwa sehemu ya Newcastle ni jambo la ajabu sana. Ni klabu ambayo sitaweza kuisahau kamwe, na nitabaki kuwa shabiki wake maisha yangu yote.
“Ninaupenda sana Uwanja wa St James’ Park. Ninapenda kucheza huko. Nadhani nguvu na hamasa ya mashabiki imekuwa sehemu muhimu sana ya maisha yangu ya soka, na nimefurahia kwa dhati kila dakika niliyocheza hapo.
“Siku yangu ya kwanza tu, watu walinipokea kwa moyo mkunjufu bila hata kuwa na wajibu wa kufanya hivyo. Sitawahi kupata maneno ya kutosha ya kuwashukuru, lakini asanteni sana,” alisema Gordon.
Winga huyo wa England amemaliza msimu akiwa mfungaji bora wa Newcastle United akipachika mabao 18, lakini hakushiriki katika mechi sita za mwisho za msimu kutokana na tetesi na mijadala kuhusu mustakabali wake.
Meneja wa Newcastle United, Eddie Howe, hapo awali alikiri kwamba hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu Gordon ndiyo iliyomweka nje ya kikosi katika sehemu ya mwisho ya msimu.
Kumuuza Gordon ni uhamisho wa pili kwa thamani kubwa zaidi katika historia ya Newcastle United, ukishika nafasi ya pili nyuma ya ule wa Alexander Isak wa Pauni 125 milioni aliyeuzwa kwenda Liverpool katika dirisha kubwa lililopita la usajili.
Mchezaji huyo pia amesema kujiunga kwake na Barcelona kumemfanya atimize ndoto zake za muda mrefu.
“Mara tu nilipojua kwamba Barcelona ilikuwa chaguo la kweli na la dhati, sikuwa na shaka hata kidogo. Ni klabu kubwa zaidi duniani. Ni jambo ambalo nimekuwa nikiota maisha yangu yote, na sasa ndoto hiyo imetimia.
“Nilizungumza na Hansi Flick (Meneja wa Barcelona), na sasa nina hamasa kubwa zaidi. Yeye ni mtu mzuri sana na mwenye uwezo mkubwa wa kusimamia wachezaji.
“Nimekuwa nikitamani kuichezea Barca tangu nilipokuwa na umri wa miaka mitatu. Kucheza pamoja na Lamine Yamal na wachezaji wengine kunanifurahisha sana. Hao ni baadhi ya wachezaji bora zaidi duniani na wana ubora wa hali ya juu. Tulipocheza dhidi yao katika Uwanja wa St James’ Park, hatukuweza hata kuumiliki mpira,” amesema Gordon.