
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeiagiza Serikali kushughulikia changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa mradi wa uwekezaji wa Bagamoyo Eco Maritime City (BEMC), ikiwemo malipo ya fidia na upatikanaji wa miundombinu muhimu.
Changamoto zilizobainika katika eneo hilo lenye hekta 9,800 lililotengwa kwa uwekezaji wa viwanda ni madai ya fidia kwa zaidi ya wananchi 3,000 katika baadhi ya maeneo, pamoja na ukosefu wa barabara, maji na umeme.
Akizungumza Bagamoyo leo Mei 30, 2026 baada ya wajumbe wa kamati hiyo kutembelea eneo la mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Damas Ndumbaro amesema endapo changamoto hizo hazitapatiwa ufumbuzi zinaweza kurudisha nyuma maendeleo yaliyokusudiwa.
“Tunaishauri Serikali kutatua changamoto hizi zinazoonekana kukwamisha mpango wa maendeleo katika eneo hili. Kama Kamati ya Bunge, tutalibeba suala hili kama azimio na kulifikisha bungeni, hususan suala la fidia kwa wananchi,” amesema Dk Ndumbaro.
Amesema kuchelewa kulipwa fidia kumewaweka wananchi wanaoishi katika maeneo husika kwenye hali ya sintofahamu kutokana na kuzuiwa kuendeleza maeneo yao.
Kuhusu miundombinu, amesema kamati hiyo itaendelea kuishinikiza Serikali pamoja na kufanya mazungumzo na mawaziri husika ili kuhakikisha huduma za barabara, maji na umeme zinapatikana kwa wakati.
Katika ziara hiyo, wajumbe wa kamati walitembelea pia ujenzi wa kiwanda cha nguo kinachoendelea kujengwa katika eneo hilo, ambapo Dk Ndumbaro amesema mradi huo ukikamilika unatarajiwa kutoa ajira kwa zaidi ya vijana 10,000.
“Ajira hizi zitawanufaisha vijana wengi na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia ulipaji kodi pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi kama usafirishaji, biashara ya chakula na huduma za mafuta,” amesema.
Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kwamba unachochea ukuaji wa sekta binafsi nchini.
“Wanaojenga viwanda hivi ni wawekezaji binafsi, si Serikali. Leo tumefika kujionea hali halisi ya maendeleo haya na kujiridhisha kwamba si maneno ya kisiasa,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Balozi Azizi Mlima amesema taasisi hiyo inakabiliwa na deni kubwa la fidia linalofikia Sh92 bilioni.
“Tunawategemea kama wadau muhimu katika mradi huu mkubwa ambao bado uko katika hatua za awali. Kwa sasa tunadaiwa fidia ya takribani Sh92 bilioni, kiwango ambacho ni kikubwa na kinaendelea kuongezeka kila mwaka,” amesema.
Dk Ndumbaro amesema kamati hiyo pia itaishauri Serikali kuunganisha mradi huo na reli ya kisasa (SGR) ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka eneo hilo kwenda maeneo mbalimbali nchini.
“Ikiwa imewezekana kujengwa reli hadi Dodoma, basi si jambo lisilowezekana kuunganisha reli kutoka Kwala hadi Bagamoyo kwa ajili ya kuimarisha uwekezaji na biashara,” amesema.
Pamoja na changamoto zilizopo, hadi Mei 2026 jumla ya wawekezaji 24 wamepatiwa maeneo yasiyokuwa na madai ya fidia na tayari wameanza utekelezaji wa miradi yao katika hatua mbalimbali.
Baadhi ya shughuli zinazoendelea ni kusawazisha maeneo, kujenga uzio, kujenga mabanda ya viwanda (industrial sheds) pamoja na kuweka miundombinu ya msingi ikiwemo barabara.