Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa na mkutano na
wasaidizi wake wakuu ili kufanya “maamuzi ya mwisho” kuhusu mfumo wa
kuongeza muda wa kusitisha mapigano na Iran, lakini ulihitimishwa bila
ufafanuzi kuhusu hatua zinazofuata.
Trump alisema Iran lazima ikubali kwamba haitawahi kuwa na
silaha ya nyuklia au bomu, ili Mlango-Bahari wa Hormuz ufunguliwe tena kwa
ajili ya “usafiri wa meli bila vikwazo kwa pande zote mbili”, na mabomu
yoyote katika njia ya maji “yaharibiwe”.
Mkutano wa Ijumaa ulifanyika katika Ikulu ya White House, katika
sehemu inayotumika kushughulikia migogoro mikubwa. Iran awali ilisema haikuwa
ikijadili kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Siku ya Alhamisi, nchi hizo mbili zilikubaliana kuhusu mfumo
wa makubaliano – unaojulikana kama mkataba wa makubaliano – ukisubiri idhini ya
Trump na uongozi wa Iran, kulingana na maafisa wa Marekani.
Inaripotiwa kwamba makubaliano hayo yangeongeza muda wa
kusitisha mapigano kwa siku 60 na kuanzisha mazungumzo kuhusu mustakabali wa
mpango wa nyuklia wa Iran.
“Rais Trump atafanya tu makubaliano ambayo ni mazuri
kwa Marekani na yanayoangazia masuala yenye kuleta utata. Iran haiwezi kamwe
kumiliki silaha ya nyuklia,” afisa mmoja wa Ikulu ya White House aliambia
CBS News, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani.
Tangu kuanzishwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano
tarehe 8 Aprili, Trump amependekeza mara kwa mara kwamba Marekani na Iran ziko
karibu kufikia makubaliano na mazungumzo yanaendelea, lakini hadi sasa hakuna
matokeo yoyote ya msingi yaliyopatikana.
Katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii mapema
Ijumaa, Trump alisema alikuwa tayari kuondoa kizuizi cha Marekani kwenye utumiaji
wa Mlango-Bahari wa Hormuz, na kuruhusu meli zilizokamatwa kwenye njia ya maji “kuanza mchakato wa ‘kuelekea nyumbani!'”
Soma zaidi:
