DAR ES SALAAM: SHIRIKA la Maendeleo Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania limesaini Hati za Makubaliano (MoUs) na taasisi tisa za elimu ya juu nchini, hatua inayolenga kuimarisha ujuzi wa vitendo, ubunifu na kuongeza fursa za ajira kwa vijana nchini.
Makubaliano hayo yameelezwa kuwa sehemu ya juhudi za muda mrefu za kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, hususan kutokana na pengo lililopo kati ya elimu ya darasani na mahitaji halisi ya soko la ajira.

Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania huzalisha takribani wahitimu 60,000 kila mwaka, lakini bado kundi kubwa la vijana hukosa nafasi za ajira au hushindwa kuingia moja kwa moja kwenye soko la kazi kutokana na kukosa uzoefu wa vitendo na uhusiano wa moja kwa moja na waajiri.
Kupitia ushirikiano huu mpya, UNDP Tanzania na vyuo husika zitashirikiana katika programu mbalimbali zikiwemo mafunzo ya ujuzi wa kazi, ushauri wa kitaaluma (mentorship), mafunzo kwa vitendo (internships), ubunifu na ujasiriamali, pamoja na utafiti wa vitendo unaolenga kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.

Taasisi zilizotia saini makubaliano hayo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Tanzania (SAUT), pamoja na taasisi nyingine za elimu ya juu zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu nchini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara, alisema vijana wanahitaji zaidi ya elimu ya darasani ili kufanikiwa katika soko la ajira.

“Mpito kutoka chuo kuingia katika maisha ya kazi haupaswi kuachwa kwa bahati. Vijana wanapaswa kuhitimu si tu wakiwa na vyeti, bali pia wakiwa na uzoefu, ujuzi wa vitendo na mwelekeo ulio wazi zaidi,” alisema Komatsubara.
Kwa upande wa taasisi za elimu ya juu, mwakilishi wao, Grace Temba kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), alisema ushirikiano huo utafungua milango mipya ya fursa kwa wanafunzi.
“Vyuo vinaweza kutoa elimu ya kitaaluma, lakini ushirikiano kama huu unasaidia kuwapa wanafunzi uzoefu, uhusiano na fursa ambazo ni muhimu katika safari yao ya maisha ya kazi,” alisema.
Mbali na makubaliano hayo, tukio hilo pia liliambatana na maonesho ya ubunifu yaliyoonesha miradi ya vijana wanaoungwa mkono na UNDP, yakionesha jinsi vijana wanavyoweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za maendeleo kupitia ubunifu na teknolojia.
UNDP Tanzania imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha vijana wanapata nafasi zaidi za kujifunza, kubuni na kushiriki moja kwa moja katika maendeleo ya taifa.
Kwa ujumla, ushirikiano huu umeelezwa kuwa hatua muhimu katika kujenga kizazi cha vijana wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.