Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Leonard Mususa amefariki dunia leo Jumamosi, Mei 30, 2026.

Taarifa iliyotolewa na familia ya marehemu imethibitisha kifo hicho na kueleza kuwa mipango ya mazishi inaendelea.

“Familia ya Mususa inakutaarifu kuhusu msiba wa Bwana Leonard Mususa uliotokea leo Jumamosi, Mei 30, 2026. Mipango ya mazishi inaendelea. Bwana ametoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kifo cha Mususa kinaacha pengo kubwa katika sekta za biashara, fedha na utawala wa kampuni kutokana na mchango wake wa muda mrefu katika taasisi mbalimbali za ndani na nje ya Tanzania.

Mususa, aliyezaliwa Septemba 25, 1953, alikuwa mhasibu mzoefu na kiongozi aliyebobea katika masuala ya usimamizi wa biashara.

Katika maisha yake ya utumishi, alijijengea heshima kubwa kutokana na utaalamu wake katika ukaguzi wa hesabu, uongozi wa taasisi na ushauri wa kimkakati kwa kampuni mbalimbali.

Marehemu aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mwananchi Communications Limited (MCL), wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, ambapo alichukua nafasi ya Zuhura Muro baada ya kumaliza muda wake wa uongozi.

Wakati wa uteuzi wake, viongozi wa MCL walimwelezea Mususa kuwa kiongozi mwenye uzoefu mkubwa ambaye angeisaidia kampuni kukabiliana na mabadiliko makubwa yaliyokuwa yakikabili sekta ya habari, ikiwemo kupungua kwa mapato ya matangazo, ushindani kutoka vyombo vingine vya habari na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL kwa wakati huo, Francis Nanai, alisema kuwa ujio wa Mususa ulikuwa muhimu kwa mustakabali wa kampuni kutokana na uzoefu wake mkubwa katika uongozi wa taasisi na biashara.

Mbali na MCL, Mususa alikuwa mmoja wa viongozi mashuhuri katika sekta ya fedha nchini. Mwaka 2024 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Selcom Microfinance Bank Tanzania Limited, nafasi aliyotarajiwa kuitumia kuimarisha utawala bora na ukuaji wa taasisi hiyo ya kifedha.

Katika taaluma yake, Mususa alikuwa Mwanachama wa Chama cha Wahasibu Wataalamu Walioidhinishwa cha Uingereza (FCCA) na Mhasibu Mtaalamu Mwandamizi aliyesajiliwa nchini Tanzania (FCPA-T).

Alijulikana kama mshauri huru wa masuala ya usimamizi na biashara, akiwa na uzoefu wa zaidi ya miongo mitatu katika sekta hiyo.

Kwa zaidi ya miaka 36, Mususa alifanya kazi katika kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa hesabu ya PricewaterhouseCoopers (PwC), ambapo alihudumu katika nyadhifa mbalimbali za juu kabla ya kustaafu mwaka 2014.

Kwa miaka 14 ya mwisho ya utumishi wake ndani ya PwC, alikuwa Country Senior Partner wa Tanzania, nafasi iliyompa jukumu la kusimamia shughuli za kampuni hiyo nchini.

Katika kipindi chote cha kazi yake, Mususa aliwahi kuhudumu katika bodi za wakurugenzi za kampuni na taasisi mbalimbali nchini Tanzania, Kenya na Mauritius. Miongoni mwa taasisi hizo ni NMB Plc, Nation Media Group Plc ya Kenya, Tanzania Breweries Plc na Reliance Insurance Company (Tanzania) Limited.

Aidha, alikuwa mmoja wa wanachama waasisi wa CEO Roundtable ya Tanzania na alihudumu kwa miaka kadhaa katika bodi ya jukwaa hilo.

Pia, aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza la Shirikisho la Viwanda na Biashara Tanzania (TCCIA), akichangia mijadala mbalimbali kuhusu maendeleo ya uchumi na mazingira ya biashara nchini.

Katika miaka ya karibuni, Mususa alikuwa mjumbe wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, aliyoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, jukumu lililolenga kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kuboresha mfumo wa kodi nchini na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Wengi waliomfahamu wanamkumbuka kama kiongozi mwenye busara, mchapakazi na aliyeamini katika uadilifu, uwajibikaji na maendeleo ya taasisi.

Uwezo wake wa kuunganisha taaluma ya uhasibu, uongozi wa biashara na maono ya maendeleo ulimfanya kuwa mmoja wa wataalamu waliokuwa wakiheshimika zaidi nchini.

Kifo chake ni pigo kwa familia, marafiki, sekta ya biashara na taasisi nyingi alizowahi kuzihudumia.

Taifa linamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika kujenga misingi ya utawala bora wa kampuni, maendeleo ya sekta ya fedha na ukuaji wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *