Dar es Salaam. Miaka 13 toka Albert Mangweha ‘Ngwea’, afariki dunia. Washikaji kibao wametupiatupia ‘masnepu’ yake mitandaoni. Alikuwa mtu wa watu, sishangai watu kuonesha utu wa kumkumbuka mtu wao. Na zaidi kilikuwa kipaji, kupita vipaji aliyasogeza maisha ya watu kwa kuwafurahisha.
LEO HII…
Ni asubuhi ninaamka ninapiga mswaki… Kisha naenda kubath kuweka mwili safi… Narudi ghetto nafungua kabati.. Nachukua pamba bring bring kwa chati… Jezi ya Arsenal na jeans ya khaki… Na chini nina simple white chata Nike… Kisha mzee najipulizia marashi… Psiiii Psiiii… Nanukia safi… Niko na machizi wa The Gunners kama laki… Tunawapigia simu COYG Camp wako wapi…”
Tangu mwaka huu uanze hakuna J’mosi bora kama hii. Na hakuna J’mosi nyingine bora huko mbele. Kama leo utajikalia ndani kwako lofa, wacha nikupe pole. Popote ulienda dunia hii tukio kubwa ni moja tu. Usiku wa Ulaya, usiku wa Arsenal. Tumejiamulia hivyo.
Hakuna kupepesa macho. Wana wote uelekeo ni mmoja tu. Nenda bar ya jirani, nenda ‘bandaumiza’ la mtaani kwako. Hii siyo siku ya kutazamia mechi chumbani ama sebuleni kwako kama mafunzo ya Mwalimu Mwakasege. Leo ni usiku wa boli.
Arteta atawaonesha na kuwajibu walimwengu. Kwamba aliiandaa timu kwa kombe siyo vinginevyo. Ni aibu mapimbi ‘Astoni Vila’, na mandezi ‘Kraisto Palesi’ wabebe ndoo za ndondo za Ulaya. Halafu ‘Asenali’ izingue kwenye ‘Yuefa’ kubwa lao? Makombe makubwa yote yanatua mwa Malkia.
‘Aseno’ ilipaka ‘vumbi la kongo’, kwa miaka 22. Hatimaye ile fleva imepatikana mwaka huu kibabe sana. Wacha ‘machizi boli tamu’ ‘tupopu shampeini’ na nyama za kuokwa. Na wale machizi boli la butua butua waendelee kuumia kibwege kama ambavyo kwa hii wiki wameteseka sana.
LEO HII…
Tunakutana mitaa ya K’nyama au Dar Village kwa party… Asubuhi tunapata zetu supu kwa chapati… Na mitungi ya kupotezea wakati… Ukitaka fegi mezani kuna pakti… Iwe spoti au esiemu au embasi… Leo utakula raha mpaka mwenyewe utasema basi…
Tunakamua mpaka ile mida ya ‘lanchi’… Tunaagiza ugali mkubwa na samaki… Makamuzi yanaendelea mpaka night… Watu wanaingia ‘greviyadi’ kwanza kupata nyasi…
Saa moja sherehe zitasimama na kuwapisha Trossard, Saka, Eze, Martineli, Gyokeres, Odegadi, Kai, Rice, Zubimendi, Saliba, Gabriel, Calafiori, Skelly, Hincapie, Jesus na wengine kama Mdueke wetu wamalize kazi tuliyowatuma. Na tulichowatuma ni makombe tu.
Balaa lote hili linaloendele Kenya, Uganda, China, Malayasia, Japan, Mbinguni (nimeambiwa huko pia masela waliotangulia mbele ya haki wala shusho la ushindi). Kwa sababu ya kukaa miaka 22 bila ubingwa ‘ipielo’. ‘So imejini” tukibeba na leo kombe ambalo hatukuwahi kubeba itakuaje?
Kuna ongezeko kubwa saaana la mashabiki wa ‘Aseno’. Huenda hii furaha inaambukiza kama tete kuwanga. Wapo ambao sikuwahi kumuona akilia na sisi wakati wa shida. Lakini hivi sasa ni ‘deile’ katupia uzi wa Gunners. Haina maana hatutaki wageni lakini pia siyo mbaya tutambuane.
Kitambaa Cheupe Mbagala huko nasikia ni mtiti. Kisuma Temeke ni mtiti, ‘Bodirumu’, ‘Jentromani’, Kitambaa ya Sinzani usipime. Ni mwendo wa tungi nyama choma na shangwe za ‘Aseno’. Kuna kitu wengi hawajajua, kwamba jamii ya kike inavutiwa zaidi na soka la ‘Aseno’ kuliko takataka zingine.
‘Ene wei’ wanangu kutoka pande zote Bongo. Ushindi wa ‘Aseno tuudediketi’ kwa ‘CowBama’ a.k.a Ngwair. Ni miaka 13 sasa msela wetu kalala pale Kihonda mitaa ya Morogoro. Huyu alikuwa ni alama sahihi ya ‘bata’, kujirusha, furaha, kukesha na kuyafanya maisha kuwa mepesi.
Muziki wake ulijieleza na kutupa picha kamili ya hulka yake. Huyu ndiye bingwa kwenye mitambao ya ‘gemu’ letu la Bongo Fleva. Ni Albert pekee ambaye angeweza kukufanya upende wimbo wa kuongelea starehe ukiwa katikati ya msiba. Alikuwa noma na nusu.
Wakati ‘Aseno’ inafika fainali ligi ya mabingwa mara ya kwanza. Ngwea alikuwa na albamu yake ya A.k.a Mimi, na singo iliyokuwa inakimbiza ni Mikasi. Miaka saba baadaye yaani 2013 akatangulia mbele ya haki. Miaka 13 baadaye toka afariki dunia ‘Aseno’ imefika fainali tena.
Tulio hai ni budi kupiga ‘saluti’ kwa ‘Saa Godi’. Kisha shukuru kwa kukupa uhai mpaka hii leo na kuona tukio hili. Wana kibao wapo ardhini nyama za miili yao zikiwa zimetafunwa na udongo. Tuliwapenda nao walitupenda, tuwaombee huku tukijua kuwa maisha ni sasa.
Ishi sasa kwani hujui ya kesho. Maisha ni sasa, hata ambaye hayupo leo aliamini atakuwepo kama wewe unavyoamini kesho utakuwepo. Nitashangaa sana kama leo utajibanza chumbani kwako kama mjusi kafiri badala ya kutoka. J’mosi hii usitegemee kama itajirudia.
LEO HII…
“Kulewa tushalewa kilichobaki mikasi… Washikaji milupo tutapata wapi? Milupo labda mitaa ya kati… So tunaenda vipi kwa miguu au kwa basi? Usiku huu bora tuchukue taxi… Poa basi tusipoteze wakati… Ksii ksii naita taxi…. Njoo utupeleke mitaa ya kati… Tukacheki midudu ya kupiga mikasi… Tuelewane kabisa itatucost shilingi ngapi?
(Buku nne tuu…) Aah wapi! Kwani hapa na pale ni umbali wa hatua ngapi? (Si mnacheki wenyewe mko wangapi?) Usimind sana babake tuko safi…”
Kuanzia bodaboda, bajaji, taksi mtandao na daladala. Maelekezo ni K’nyama Viwanja vya Posta. Na kama upo mbali jichanganye maeneo yako na wana.
Leo ndiyo sikukuu kuliko Xmass na Eid, ni ‘holidei siizoni’ kimsingi. ‘Aseno’ imetupa ‘stresi’ kwa miaka 22, ni haki yetu kufurahia.
“Tuchangeni tusipoteze wakati…
Ludi eh kwani we una shilingi ngapi? Buku tano… Venture? Bati… Sasa wewe una bati usiku huu unaenda wapi… Wakati hiyo bati hata soda tuu hupati… Bora uweke kesho unywee chai na chapati… Asiye na kitu mi naona bora akabaki… Tusije mbele tukashikana mashati… Suka eh! tuanzie Masaki… Mchizi kapiga simu yani kuna bonge la party…”
‘Resti ize Albatinyo’. Wanao leo tunashangweka na ubingwa wa ‘Aseno’ kibabe sana. Ni mwendo wa ‘kubrezi’ na kupitisha kooni vigumu na vichungu. Madhara yake ni kesho na hatujutii. Kanuni ni ileile kama uliyoacha. Tuishi na maisha ni sasa. Kesho yetu ni majaaliwa.