DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeahidi kuwa kuwa itandelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na ugonjwa wa Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (MSY) kwa kuwezesha mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wake.
Hayo yamebainishwa na mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Shigela Malosha wakati wa ufunguzi wa mafunzo kuhusu afya na ustawi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Ijumaa (Mei 29, 2026).
Akizungumza katika tukio hilo, Shigela alisema kuwa kufanyika kwa mafunzo hayo ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na PURA katika kufanikisha utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Virusi Vya Ukimwi (VVU), UKIMWI na MSY mahala pa kazi.

“Kupitia mafunzo haya tutaongeza uelewa wa watumishi wa PURA kuhusu VVU, UKIMWI na magonjwa sugu yasiyoambukiza hivyo kuendelea kuunga mkono juhudi Serikali katika eneo hili.
“Vile vile, kwa kutoa mafunzo haya, PURA inachangia moja kwa moja utekelezaji wa nguzo ya pili ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuwa na jamii yenye afya” aliongeza Shigela.
Mafunzo hayo yaliyotolewa na wataalamu wabobezi wa masuala ya afya yalihusisha masuala mengine ikiwemo afya ya akili, lishe bora, usimamizi wa masuala ya kifedha na elimu kuhusu mfuko wa hifadhi ya jamii.
Sambamba na mafunzo hayo, watumishi wa PURA walipata fursa ya kupima afya kupitia huduma za uchunguzi zilizotolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Huduma hizo zilijumuisha upimaji wa VVU, homa ya ini, magonjwa ya moyo, sukari, presha pamoja na uzito wa mwili.
Aidha, wafanyakazi walipata ushauri wa kitaalamu kuhusu matokeo ya vipimo vyao ili kuwawezesha kuchukua hatua stahiki za kuboresha afya zao.
Vile vile, huduma ya chanjo dhidi ya homa ya ini ilitolewa kwa wafanyakazi waliokuwa tayari kupata chanjo hiyo kama sehemu ya hatua za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.