MAKAMU Mwenyekiti wa Barberian FC, Robert Munis amesema hatoondoka katika timu hiyo hata kama itashuka daraja na kwenda kushiriki Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao, licha ya presha kubwa iliyopo kwa viongozi na wachezaji wa kikosi hicho.

Munis aliyewahi kushika wadhifa huo wa makamu mwenyekiti akiwa na kikosi cha maafande wa Polisi Tanzania, amejiunga na Barberian FC zamani Kiluvya United, huku akikabiliwa na kibarua kigumu cha kuipambania timu hiyo ili isishuke daraja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Munis amesema licha ya nafasi mbaya iliyopo timu hiyo kwa sasa ila wataendelea kupambana kwa mechi zilizobakia, ila ikitokea ikashuka atabaki na kuunda mikakati mipya kwa lengo la kutengeneza kikosi cha ushindani.

“Kwa nafasi tuliyopo ni ngumu sana kubakia kwa sababu ya mwenendo wetu usioridhisha, niwahakikishie tu mashabiki zetu tuendeleze umoja na tusigawanyike, tuna timu nzuri sana lakini tunahitaji kujipanga zaidi msimu ujao,” amesema Munis.

Munis ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) na Mjumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amesema bado hawajakata tamaa japo ni ngumu kwa kikosi hicho kukinusuru kwa sasa.

Barberian ambayo zamani ilikuwa inajulikana kwa jina la Kiluvya United, katika mechi 27 ilizocheza hadi sasa msimu huu, imeshinda moja tu, sare tisa na kupoteza 17, ikifunga mabao 15 na kuruhusu 41, ikishika nafasi ya 15 na pointi zake 12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *