Kiungo mshambuliaji wa Kitanzania anayekipiga katika klabu ya She Corporate FC ya Uganda, Husna Mpanja, amesema anaamini muda wake wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini humo utafika licha ya kushindwa kufanikisha ndoto hiyo msimu huu.

She Corporate ilimaliza msimu ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi baada ya kukusanya pointi 51, pointi moja nyuma ya mabingwa wapya, Kawempe Muslim Women FC waliomaliza kileleni wakiwa na pointi 52.

Tofauti hiyo ndogo ya pointi moja imeendelea kumuumiza Mpanja ambaye alikiri kikosi hicho kilikuwa na matumaini makubwa ya kutwaa taji kabla ya msimu kumalizika.

MPA 01

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kumalizika kwa ligi hiyo, Mpanja amesema ingawa wamekosa ubingwa, bado anaona kuna mengi ya kujivunia kutokana na kiwango walichoonyesha msimu mzima.

“Kwa kweli tulikuwa na imani kubwa ya kushinda ubingwa msimu huu, lakini ndiyo mpira. Tumepambana mpaka mwisho na tofauti imekuwa pointi moja tu. Inaumiza, lakini tunapaswa kukubali matokeo,” amesema Mpanja.

Nyota huyo wa Tanzania amesema kilichobaki sasa ni kujipanga kwa ajili ya msimu ujao huku akiahidi kurejea akiwa na nguvu zaidi ili kuhakikisha ndoto ya kubeba ubingwa inatimia.

MPA 02

“Hii ni changamoto kwetu. Tutarudi tukiwa imara zaidi kwa sababu bado tuna malengo makubwa. Nitaendelea kufanya kazi kwa bidii ili msimu ujao tuweze kufikia kile tulichokikosa safari hii,” amesema.

Msimu huu Mpanja alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi cha She Corporate, akisaidia timu hiyo kubaki kwenye mbio za ubingwa hadi dakika za mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *