KAMA kuna jambo ambalo limekuwa likivutia macho ya mashabiki wa soka kila wakati wachezaji wa Timu ya Taifa, Taifa Stars wanapoingia kambini, basi ni namna kiungo wa Shamakhi FC ya Azerbaijan, Alphonce Mabula anavyopenda kutokeleza kwa mavazi yake.

Mabula amekuwa miongoni mwa nyota wanaovaa mitoko tofauti, jambo ambalo mara nyingi huzua mijadala mitandaoni kuhusu aina ya mavazi anayochagua kabla ya kuungana na wenzake kambini.

Akizungumza na Mwanaspoti, kiungo huyo amesema kuvaa vizuri ni sehemu ya maisha yake na amekuwa akitumia muda kuchagua mavazi yanayolingana na muonekano anaoutaka.

MABU 01

“Kwangu kupendeza ni jambo la muhimu. Mara nyingi nafikiria ni nguo gani itanifaa kwa wakati husika, kisha nikiingia dukani nachagua kile ninachokipenda na kukinunua,” amesema Mabula.

Nyota huyo alikiri amekuwa akivutiwa na namna beki wa Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa, Jules Kounde anavyopendeza nje ya uwanja, jambo linalompa msukumo wa kujaribu mitindo mbalimbali ya mavazi.

“Ninamfuatilia sana Kounde ni mchezaji ambaye anapenda fasheni na mara nyingi anaonekana na mavazi ya kipekee. Nimekuwa nikijifunza vitu mbalimbali kwa namna anavyovaa hususan akiwa anaingia kambini,” amesema Mabula.

Kuhusu kiwango cha fedha anachotumia kununua mavazi, Mabula amesema huwa haangalii sana bei endapo akipenda nguo, akisisitiza  kilicho muhimu kwake ni ubora na namna nguo hiyo itakavyompendeza.

“Nikiona nguo nimeipenda, ninainunua siangalii sana bei. Mavazi yangu mengi nanunua Ulaya, hivyo ni kweli gharama zake huwa si ndogo, lakini sipendi kuweka wazi kiasi halisi ninachotumia.”

MABU 02

Kiungo huyo fundi huu ni msimu wake wa pili kuitumikia Ligi Kuu Azerbaijan akicheza mechi 28 kwa dakika 1,739 akifunga mabao mawili. Msimu wa kwanza 2024/25 alipoingia dirisha dogo akitokea Sp. Subotica ya Serbia alicheza mechi 17 akifunga mabao matatu.

Mabula ambaye amekuwa akitumika kwenye nafasi mbalimbali za kiungo mkataba wake na Shamakhi unatamatika June 30 mwaka huu na tayari kuna baadhi ya timu zimeanza kupeleka ofa kuhitaji saini yake ikiwemo Kasımpasa Spor Kulubu ya Uturuki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *