Kibaha. Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amezitaka taasisi zilizohusika katika utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya TBPL, TFC,TARI, TFRA na TPHPA kuhakikisha zinatekeleza kwa vitendo na masharti yote yaliyomo katika makubaliano hayo ili kuleta manufaa kwa Serikali, wakulima na wananchi kwa ujumla.

Waziri Kapinga ametoa agizo hilo Mei 30, 2026 wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo iliyofanyika katika Kiwanda cha Viuadudu cha TBPL kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Alisema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya viwanda na kilimo nchini kwa kuwa utasaidia kuongeza uzalishaji, usambazaji na upatikanaji wa masoko ya ndani na kimataifa kwa mbolea hai inayozalishwa na kiwanda hicho.

“Ni muhimu kwa kila taasisi iliyosaini makubaliano haya kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi na kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa. Serikali inatarajia kuona matokeo chanya yatakayochochea ukuaji wa sekta ya kilimo, kuongeza uzalishaji wa viwandani na kuinua kipato cha wakulima,” alisema Kapinga.

Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa za ndani ili kuongeza ushindani katika soko la kikanda na kimataifa.

Kapinga alisema pamoja na kuzalisha mbolea hai, kiwanda hicho kinazalisha bidhaa mbalimbali muhimu zikiwemo dawa za kuangamiza mazalia ya mbu ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika juhudi za kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na mbu.

Aidha, aliwataka viongozi na watendaji wa taasisi zinazohusika kuzingatia utendaji wenye tija na uwajibikaji ili kuhakikisha kiwanda kinaendelea kujiendesha kwa ufanisi na kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwanda vya Mbolea Tanzania (TFC), Samuel Mshote, alisema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta ya viwanda katika kuimarisha upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo.

Alisema ushirikiano huo utasaidia kuongeza matumizi ya mbolea hai nchini, kuboresha afya ya udongo, kuongeza tija kwa wakulima na kupunguza gharama za uzalishaji wa mazao.

“Mkataba huu una manufaa makubwa kwa wakulima na Serikali kwa ujumla. Kupitia ushirikiano huu tutaimarisha tafiti, usajili, udhibiti wa ubora na upatikanaji wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. Hii itasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, kukuza mapato ya wakulima na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema Mshote.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Nicolaus Shombe, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuliwezesha shirika hilo kusimamia na kuendeleza viwanda mbalimbali vya kimkakati nchini.

Alisema msaada unaotolewa na Serikali umewezesha NDC kuimarisha uzalishaji viwandani, kuongeza ajira kwa Watanzania na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.

“Tunatoa shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kutuamini na kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu. Tutaendelea kusimamia viwanda kwa ufanisi, kuzingatia misingi ya uwajibikaji na kuhakikisha uwekezaji uliofanywa unaleta matokeo chanya kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” alisema Shimbe.

Aliongeza kuwa NDC itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha viwanda vilivyo chini ya usimamizi wake vinaongeza uzalishaji, ubora wa bidhaa na ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Historia fupi ya kiwanda cha viuadudu cha TBPL

Kiwanda cha Viuadudu cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) kilichopo Kibaha mkoani Pwani ni moja ya viwanda vya kimkakati vinavyosimamiwa na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC). Kiwanda hicho kilianzishwa kwa lengo la kuzalisha bidhaa za kibayolojia zinazosaidia sekta za afya na kilimo.

Miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho ni dawa za kuangamiza mazalia ya mbu zinazotumika katika kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na mbu pamoja na mbolea hai inayosaidia kuboresha rutuba ya udongo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Kupitia uzalishaji wake, kiwanda hicho kimechangia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi, kuokoa fedha za kigeni, kuongeza ajira kwa Watanzania na kuchochea maendeleo ya sekta za afya na kilimo.

Serikali inaendelea kukiimarisha kiwanda hicho ili kiweze kuongeza uzalishaji na kupanua masoko ya bidhaa zake ndani na nje ya Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *