Dar es Salaam. Ili kukuza na kuongeza uwezo wa suluhisho zinazoongozwa na wabunifu wa ndani, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na StartHub Africa, limezindua shindano la ubunifu linalolenga kutambua na kusaidia biashara na wabunifu wenye uwezo wanaofanyia kazi suluhisho endelevu za mifumo ya chakula.

Shindano hilo lililopewa jina la Ignite linaangazia maeneo mawili muhimu: suluhisho za matumizi bora ya maji katika uzalishaji wa chakula na vyakula vya nyongeza vyenye lishe kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi miezi 59.

Waandaaji wanazialika kampuni changa bunifu (Startups), biashara ndogo na za kati, wabunifu, na taasisi mbalimbali kuendeleza suluhisho zinazoweza kukua na kutekelezeka kwa vitendo ili kuongeza ustahimilivu kwa jamii, kuimarisha mifumo ya chakula ya ndani na kuongeza upatikanaji wa lishe.

Kwa mujibu wa WFP Tanzania, lengo la shindano hilo siyo tu kutambua mawazo ya kibunifu, bali pia kusaidia suluhisho zenye uhalisia wa kutekelezwa na kukua kwa kiwango kikubwa zaidi.

Washiriki watakaochaguliwa watanufaika na mafunzo ya kitaalamu, msaada wa maendeleo ya biashara, fursa za kuunganishwa na wadau wa mfumo wa ubunifu, pamoja na ufadhili wa mpaka Dola za Marekani 40,000 (Sh105.1 milioni) kwa ajili ya hatua ya awali ya ukuaji na kuimarisha ubunifu wao.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Mkuu wa Ubunifu wa WFP Tanzania, Tayamika Mattao amesema IGNITE Challenge inaonyesha umuhimu unaokua wa ubunifu unaoongozwa na wadau wa ndani katika kukabiliana na changamoto za mifumo ya chakula na mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania.

“Tanzania tunaendelea kuona wabunifu wakibuni suluhisho zenye manufaa makubwa kwa jamii, hasa katika sekta za kilimo, lishe, na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Kupitia Ignite Challenge, tunataka kutengeneza fursa kwa wabunifu hawa kupata msaada, ushirikiano, na rasilimali zinazohitajika ili kukuza mawazo yao na kuchangia katika kujenga mifumo ya chakula iliyo imara na endelevu,” amesema Mattao.

Shindano hilo linakuja katika kipindi ambacho Tanzania, kama ilivyo kwa mataifa mengi duniani, inaendelea kukabiliwa na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi zinazoathiri mifumo ya uzalishaji wa chakula sambamba na changamoto za lishe kwa makundi yaliyo hatarini kama watoto walio chini ya miaka mitano.

Kwa wabunifu wanaoendeleza suluhisho za kilimo zinazotumia maji kwa ufanisi ili kuimarisha mifumo endelevu ya chakula katika shule na kambi za wakimbizi, kuboresha upatikanaji wa maji, kuongeza ufanisi wa umwagiliaji pamoja na uzalishaji wa chakula unaozingatia mabadiliko ya tabianchi, Ignite Challenge inatoa fursa ya kujaribu, kuboresha na kukuza suluhisho zao kwa manufaa mapana.

Vilevile, wazalishaji au wasambazaji wa vyakula wenye uwezo wa kuzalisha vyakula vyenye lishe kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi miezi 59 wanahamasishwa kutuma maombi yao ili kusaidia kuboresha matokeo ya lishe kwa watoto Tanzania.

Mpango huo, pia, unaonyesha mwelekeo unaokua wa mifumo ya ubunifu inayoongozwa na wadau wa ndani, ambapo wajasiriamali, taasisi za utafiti, wadau wa maendeleo pamoja na sekta binafsi wanashirikiana kutengeneza suluhisho zinazokidhi mahitaji halisi ya jamii.

Kupitia shindano hilo, WFP kwa kushirikiana na StartHub Africa, inalenga kuimarisha mfumo wa kukuza ubunifu na kusaidia biashara zenye matumaini ya kuchangia mifumo endelevu na imara ya chakula nchini Tanzania.

Maombi ya kushiriki kwenye shindano la Ignite Challenge Tanzania 1.0 tayari yamefunguliwa rasmi na waombaji wanatakiwa kutuma maombi yao kabla ya Ijumaa, Juni 5, 2026, kupitia tovuti ya www.starthubafrica.org/ignite.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *