Hai. Baadhi ya waendesha bodaboda na bajaji wa Stendi ya Sanya wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kuweka utaratibu wa mikopo nafuu ya pikipiki na bajaji ili waweze kumiliki vyombo vyao vya kazi na kuongeza kipato.

Ombi hilo limetolewa leo Jumapili Mei 31, 2026 na Mwenyekiti wa Shina la Wakereketwa Vijana wa Bajaji na Bodaboda Stendi Ndogo ya Sanya Juu, Joseph Masawe, wakati wa uzinduzi wa shina hilo uliofanywa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi.

Masawe amesema shina hilo lina wanachama 78, kati yao 39 ni waendesha bajaji na 39 waendesha bodaboda, huku wengi wao wakitumia vyombo vya watu wengine.

Amesema hali hiyo inawalazimu kutumia sehemu kubwa ya mapato yao kulipa makubaliano ya kila siku kwa wamiliki wa vyombo hivyo na kubaki na kipato kidogo kisichokidhi mahitaji yao muhimu.

“Tunaiomba Serikali na CCM kutusaidia kupata mikopo nafuu ya pikipiki na bajaji ili vijana waweze kumiliki vyombo vyao wenyewe, kuongeza kipato na kujitegemea kiuchumi,” amesema Masawe.

Amesema uwezeshaji huo utasaidia kuongeza ajira kwa vijana, kuboresha maisha yao na kuimarisha mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

“Tunawaahidi viongozi wetu kuwa vijana wa bodaboda na bajaji wa Sanya tutakuwa mstari wa mbele kukijenga na kukiimarisha CCM pamoja na kuhamasisha vijana wengine kushiriki shughuli za maendeleo,” amesema.

Akizungumza baada ya kuzindua shina hilo, Kihongosi amesema CCM inaendelea kutambua mchango wa vijana katika uchumi wa nchi na itaendelea kusikiliza changamoto zao ili kutafuta ufumbuzi.

Amesema suala la vijana wa bodaboda na bajaji limepewa uzito ndani ya chama hicho na kuahidi kufuatilia changamoto zao kwa karibu.

“Nitakupa namba yangu ya simu. Ukiona kuna changamoto yoyote inayowahusu vijana wa bodaboda na bajaji, nipigie simu moja kwa moja. Mimi pamoja na wenzangu tutatafuta suluhisho,” amesema Kihongosi.

Amesema lengo la Serikali na CCM ni kuhakikisha vijana wanapata fursa za kujiajiri na kuboresha maisha yao kupitia kazi halali wanazozifanya.

Kwa mujibu wa Kihongosi, maendeleo yanayoonekana katika Wilaya ya Hai na maeneo mengine nchini yametokana na utekelezaji wa sera, mipango na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Katika ziara hiyo, Kihongosi pia alikagua Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Hai ambapo Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa halmashauri hiyo, Dk Itikija Msuya, amesema hospitali hiyo imepata maboresho makubwa ya miundombinu katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Amesema majengo sita mapya yamejengwa yakiwemo ICU, maabara ya kisasa, wodi ya wajawazito, famasi pamoja na njia za kuunganisha majengo yote ya hospitali.

Aidha, amesema hospitali imepokea vifaa tiba vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya Sh550 milioni, ikiwemo mashine ya kisasa ya X-Ray.

Dk Msuya amesema wodi maalumu ya watoto wachanga iliyoanzishwa mwishoni mwa mwaka 2025 imehudumia watoto zaidi ya 200 bila kurekodi kifo chochote, huku Wilaya ya Hai ikifanikiwa kutokuwa na kifo cha mama mjamzito mwaka 2025.

Hata hivyo, amesema hospitali bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa watumishi 113, ukosefu wa jengo la kisasa la upasuaji na kutokuwa na uzio wa kutenganisha wagonjwa wa ndani na wa nje.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *