Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limezitaka kampuni zinazofanya kazi za bandari nchini kugeukia nishati safi katika kuendesha shughuli zao za kila siku ili kupunguza uzalishaji hewa ukaa.
Wito huo umetolewa leo Juni Mosi, 2026 jijini Dar es Salaam na Ofisa Mazingira kutoka NEMC, Jackline Wikechi wakati wa uzinduzi wa mtambo wa kunyanyulia makontena (Reach Stacker) unaotumia umeme katika bandari kavu ya Azam (Azam ICD).
Teknolojia hiyo ni mpya barani Afrika kwani mitambo mingi ya aina hiyo inatumia mafuta ya dizeli, takribani lita 200 kwa siku, jambo linalochochea uchafuzi wa mazingira kutokana na hewa ukaa inayozalishwa wakati linafanya kazi.
Wikechi amesema kuwepo kwa mtambo (crane) huo itasaidia kupunguza hewa ukaa pamoja na kelele zinazozalishwa katika eneo la kazi na maeneo ya jirani.
“Niombe kampuni nyingine ziige mfano wa kampuni ya Bakhresa (SSB) kwa kugeukia nishati safi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Teknolojia katika mtambo huu ni rafiki kwa mazingira na NEMC tunaiunga mkono,” amesema ofisa huyo.
Ameongeza kwamba Tanzania ilisaini mkataba wa kimataifa unaotaka kupunguza uchafuzi wa mazingira katika shughuli za bandari, hivyo amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa mkataba huo wa kimataifa.
“Mtambo huo utapunguza matumizi ya mafuta ambapo crane za mafuta zinatumia lita 200 za dizeli kwa siku. Pia, mtambo huu utapunguza uvujaji wa mafuta anayotoka kwenye mitambo,” amesema ofisa mazingira huyo wa NEMC.
Akizungumzia mtambo huo, Meneja Mkuu wa Azam ICD, Issa Ahmed Jaye amesema mtambo huo wa kisasa unaotumia umeme, unachajiwa kwa saa moja hadi mbili ambapo unafanya kazi kwa saa nane.
Amesema mashine hiyo iliyogharimu Dola za Marekani 500,000 (Sh1.3 bilioni), imesaidia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kwani kwa siku moja mtambo wa dizeli unatumia lita 180 hadi 200, sawa na Sh700,000 kwa bei ya sasa, lakini mtambo huo wa umeme ukichajiwa ukatumika kwa saa nane, gharama yake haizidi Sh100,000.
“Ujio wa mtambo huu umekuwa faraja kwetu kwa kuwa bei ya mafuta imepanda, kwa hiyo umefika kwa wakati mwafaka. Pia, tunaunga mkono jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi,” amesema Jaye.
Awali akizindua mtambo huo pekee uliopo Tanzania, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB), Ally Mukadam amesema uwekezaji huo unadhihirisha dhamira yao ya dhati katika utunzaji wa mazingira maendeleo endelevu ya kiuchumi na kimazingira.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji, ubunifu na biashara hapa nchini. Mtambo huu ni kielelezo cha kujizatiti kwetu katika suala la uhifadhi wa mazingira,” amesema Mukadam.