Dar es Salaam. Kwa zaidi ya miaka 100 tangu kugunduliwa kwa insulini mwaka 1921, wagonjwa wa kisukari, hasa aina ya kwanza (Type 1), wamekuwa wakitegemea sindano za insulini kuishi.

Hata hivyo, maendeleo ya hivi karibuni kutoka China yameibua matumaini kwamba siku moja baadhi ya wagonjwa wanaweza kuishi bila sindano hizo.

Watafiti wa Chuo Kikuu cha Peking na taasisi nyingine za utafiti nchini China wamefanikiwa kutumia teknolojia ya seli shina (stem cells) kutengeneza seli zinazofanana na zile za kongosho zinazozalisha insulini.

Seli hizo hupandikizwa mwilini mwa mgonjwa kwa lengo la kurejesha uwezo wa mwili kudhibiti kiwango cha sukari katika damu kwa njia ya asili.

Kilichovutia zaidi ni matokeo ya mgonjwa mwenye umri wa miaka 25 aliyekuwa na kisukari aina ya kwanza. Baada ya kupandikizwa seli hizo, mwili wake ulianza kuzalisha insulini ya kutosha kiasi cha kutohitaji tena sindano za insulini kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Hii ni hatua kubwa kwa sababu kisukari aina ya kwanza hutokea pale mfumo wa kinga unapoharibu kabisa seli zinazozalisha insulini.

Kwa wagonjwa wa kisukari aina ya pili, ambao ndio wengi zaidi duniani, teknolojia hiyo pia imeonyesha uwezo wa kuboresha uzalishaji wa insulini na udhibiti wa sukari mwilini. Katika baadhi ya majaribio, wagonjwa walipunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya dawa na insulini.

Akizungumzia mafanikio hayo leo Juni Mosi, 2026 Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Ndani na Kisukari, Profesa Kaushik Ramaiya, anasema utafiti wa kutumia seli shina kurejesha uzalishaji wa insulini si jambo jipya kabisa katika ulimwengu wa sayansi, lakini changamoto kubwa imekuwa namna ya kuhakikisha seli zinazopandikizwa zinakubalika na mwili wa mgonjwa.

Anasema kwa miaka kadhaa watafiti katika nchi mbalimbali wamekuwa wakijaribu kutengeneza au kupandikiza seli zinazoweza kuzalisha insulini, lakini mara nyingi mfumo wa kinga wa mwili huzitambua kama vitu vya nje na kuzishambulia au kuzikataa.

“Kimsingi watafiti wamekuwa wakitafuta njia ya kuingiza seli zinazoweza kuzalisha insulini ili kuchukua nafasi ya zile zilizoharibika. Changamoto kubwa imekuwa mwili kuzikataa kwa sababu unaona ni vitu vya nje. Hilo ndilo limekuwa kikwazo kikubwa katika tafiti nyingi zilizofanyika hapo awali,” anasema Profesa Ramaiya.

Anasema kinachovutia katika utafiti wa China ni matumizi ya seli zilizotokana na mgonjwa mwenyewe, jambo linaloweza kupunguza hatari ya mwili kuzikataa baada ya kupandikizwa.

Hata hivyo, anaonya bado ni mapema kutangaza kuwa kisukari kimepatikana tiba ya kudumu kwa kuwa tafiti hizo ziko katika hatua za majaribio na zinahitaji kuthibitishwa kwa idadi kubwa zaidi ya wagonjwa.

“Kwa kawaida tafiti huanza maabara, zikionyesha mafanikio huendelea kwenye majaribio ya binadamu kwa hatua mbalimbali. Matokeo ya awali yanaonekana kuwa na matumaini, lakini bado watafiti wanapaswa kuthibitisha usalama wake wa muda mrefu na kuona kama teknolojia hiyo inaweza kutumika kwa watu wengi zaidi,” anasema.

Ameongeza ikiwa teknolojia hiyo itafanikiwa katika majaribio makubwa, inaweza kufungua ukurasa mpya wa matibabu ya kisukari kwa kurejesha uwezo wa kongosho kuzalisha insulini badala ya wagonjwa kutegemea dawa au sindano maisha yao yote.

Utafiti wa awali wa timu ya Profesa Deng Hongkui wa Chuo Kikuu cha Peking ulihusisha wagonjwa watatu wa kisukari aina ya kwanza (Type 1) waliopandikizwa seli zilizotokana na seli shina zao wenyewe.

Mgonjwa wa kwanza, mwanamke wa miaka 25, aliacha kutumia insulini baada ya miezi miwili na nusu, huku wagonjwa wengine wawili wakiendelea kufuatiliwa.

Mei mwaka 2026, timu nyingine ya watafiti wa Shanghai imeripoti wagonjwa watatu wa kisukari aina ya kwanza waliotibiwa kwa teknolojia ya “E-islet” iliyotokana na seli shina, wakionyesha kurejea kwa kazi ya kongosho.

Pia kulikuwa na taarifa ya mgonjwa mmoja wa kisukari aina ya pili aliyefanikiwa kuacha insulini baada ya kupandikizwa seli zilizotengenezwa kutoka seli shina zake mwenyewe. Hata hivyo, hii ilikuwa kesi ya mtu mmoja katika hatua za majaribio.

Hadi sasa, mafanikio yaliyoripotiwa China yanahusisha wagonjwa wachache katika majaribio ya kliniki ya awali, na si tiba iliyothibitishwa kwa matumizi ya watu wote wenye kisukari.

Mafanikio hayo, yaliyochapishwa katika majarida ya kisayansi ya Cell na Cell Discovery, yameibua matumaini mapya kwa mamilioni ya wagonjwa duniani wanaotegemea sindano za insulini au dawa za kudhibiti kiwango cha sukari katika damu.

Kisukari aina ya kwanza hutokea pale mfumo wa kinga ya mwili unaposhambulia na kuharibu seli za kongosho zinazozalisha insulini. Bila homoni hiyo, sukari hukusanyika kwenye damu na kusababisha madhara makubwa ikiwamo upofu, ugonjwa wa figo, uharibifu wa mishipa ya fahamu na kukatwa viungo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *