
Hanang’. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekemea tabia ya kiburi cha madaraka, migawanyiko na kutanguliza masilahi binafsi ndani ya chama na Serikali, kikieleza kuwa hali hiyo inadhoofisha utendaji na kupunguza kasi ya maendeleo kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 1, 2026 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi wa Masakta wilayani Hanang, mkoani Manyara, katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi Kanda ya Kaskazini.
Kihongosi amesema viongozi wa chama na Serikali wanapaswa kudumisha upendo, umoja na mshikamano, huku wakitambua kuwa nafasi walizonazo zinatokana na chama.
“Dumisheni upendo, umoja na mshikamano. Hakuna aliye mkubwa kuliko chama. Kiburi cha madaraka kisiwepo, migawanyiko isiwepo na masilahi binafsi yasitawale, kwani mambo hayo yanaweza kudhoofisha chama na Serikali,” amesema.
Amesema viongozi wanapaswa kushirikiana na kuweka mbele maslahi ya wananchi ili kuimarisha utendaji na kuharakisha maendeleo.
Katika ziara hiyo, Kihongosi alikagua mradi wa chujio la maji katika Kijiji cha Jorodom wenye thamani ya Sh1.1 bilioni uliokamilika mwaka 2025 na unaowanufaisha zaidi ya wananchi 35,000 kwa huduma ya maji saa 24 kwa siku.
Amesema mradi huo una uwezo wa kuzalisha lita milioni 2.5 za maji kwa siku na umechangia kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo, hususan baada ya maafa ya maporomoko ya tope yaliyotokea Hanang mwaka 2023.
Pia amesisitiza kuwa CCM itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, huku akipongeza watumishi wa Serikali kwa usimamizi wa mradi huo.
Mmoja wa wananchi wa eneo hilo, Catherine Hayuma, amesema kukamilika kwa mradi huo kumemaliza adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali iliyokuwa imeongezeka baada ya maafa ya mwaka 2023.