Dar es Salaam. Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema Ofisi hiyo haikionei Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), bali inasimamia utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa bila upendeleo kwa chama chochote.

Amesema wingi wa barua inazokiandikia Chadema kuhitaji maelezo kuhusu kauli za viongozi wake hauwezi kutumika kama kigezo cha kuonyesha kuwa chama hicho kinaonewa na ofisi hiyo.

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa,Sisty Nyahoza (kushoto) akiagana na Naibu Katibu Mkuu Bara Chadema, Amani Ngolugwa  baada ya kumaliza kikao na viongozi wa Chadema, kilichofanyika Makao Makuu ya chama hicho,jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga

Kauli hiyo imekuja wakati ambapo Chadema na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa zimekuwa katika mvutano wa muda mrefu, unaohusisha kuandikiana barua na kutoa kauli kupitia vyombo vya habari, huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kwa masuala mbalimbali.

Kwa muda mrefu, Chadema imekuwa ikituhumiwa na Ofisi ya Msajili kwa madai ya kukiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019, baadhi ya tuhuma hizo zinahusu viongozi wake kutoa kauli zinazotafsiriwa kuwa za matusi au zinazokiuka misingi ya sheria na Katiba ya nchi.

Kwa upande wake, Chadema imekuwa ikijibu barua hizo huku ikiikosoa Ofisi ya Msajili kwa madai ya matumizi mabaya ya mamlaka, pamoja na kuendesha mikakati inayolenga kukidhoofisha chama hicho na kufanya maamuzi yasiyo na manufaa kwa umma.

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, Chadema ilipokea barua mbili za kutakiwa kujieleza kwa nini isichukuliwe hatua za kisheria, ikiwemo kufutiwa usajili au kutozwa faini, kutokana na kauli zinazodaiwa kutolewa na baadhi ya viongozi wake katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Juni 1, 2026, baada ya kutembelea Makao Makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam kujionea utekelezaji wa dawati la jinsia na sera ya jinsia ya chama hicho, Nyahoza amesema utoaji wa barua za kujieleza haupaswi kutafsiriwa kuwa ni uonevu.

“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni mlezi wa vyama vyote vya siasa. Vyama vyote ni watoto wetu na hatumpendelei mtu yeyote. Ndio maana tumekuja hapa Chadema na tumepokelewa vizuri. Kama tungekuwa na uhusiano mbaya nao, tusingepokelewa namna hii. Kazi yetu ni kuvilea vyama vyote na kuvielekeza pale panapojitokeza changamoto,” amesema Nyahoza.

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza (wapili kulia) akiwa kwenye kikao na viongozi wa Chadema,jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga

Amesema njia bora kwa vyama vya siasa kuepuka kuandikiana barua mara kwa mara na Ofisi ya Msajili ni kuzingatia kikamilifu sheria ya vyama vya siasa pamoja na masharti ya usajili.

“Kama walezi wa vyama vya siasa, tunavihimiza vyama vyote kuzingatia sheria ya vyama vya siasa na masharti ya usajili katika shughuli zao zote za kisiasa na kichama, ikiwemo mikutano ya hadhara inayofanyika kote nchini,” amesema.

Nyahoza amesema ofisi yake inatekeleza majukumu kwa mujibu wa sheria bila upendeleo wala ubaguzi, akieleza kuwa kifungu cha nne na cha tano cha sheria husika vinaipa mamlaka ya kutekeleza wajibu wake kwa uhuru.

Akijibu swali kuhusu sababu ya Chadema kuandikiwa barua nyingi za kujieleza, Nyahoza amesema idadi ya barua si kipimo sahihi cha kutathmini uhusiano kati ya chama na ofisi hiyo.

“Huwezi kupima jambo kwa kuangalia wingi wa barua zinazoandikwa. Muhimu ni kuangalia sababu iliyosababisha barua hiyo kuandikwa, hatuionei Chadema amesema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, Aman Golugwa, ameitaka Ofisi ya Msajili kuacha kile alichodai tabia ya kuvujisha barua zinazoelekezwa kwa chama hicho kabla hazijafikishwa rasmi.

“Haiwezekani barua inaandikwa kwa Chadema lakini vyombo vya habari vinakuwa tayari vinafahamu maudhui yake kabla hatujaipokea au kuisoma. Hilo ni jambo linalozua maswali mengi,” amesema Golugwa.

Akizungumza mbele ya Nyahoza, Golugwa ameitaka ofisi hiyo kuzingatia weledi katika masuala ya kiutawala na kuhakikisha vyama vyote vinatendewa kwa usawa.

“Tumezungumza mambo mengi kuhusu namna ya kushughulikia barua hizi za kujieleza, lakini baadhi ya masuala hayo yanabaki kuwa ya ndani,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *