Dar es Salaam. Wanafunzi 246,197 wakiwemo wasichana 114,102 na wavulana 132,095 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi mwaka 2026.

Kati ya wanafunzi hao 631 ni wenye mahitaji maalumu.

Idadi hiyo ni ongezeko kidogo ikilinganishwa na wanafunzi 214,141 waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano na vyuo vya ufundi mwaka jana ambapo kati yao 1,028 walikuwa ni wenye mahitaji maalumu.

Akitoa taarifa hiyo leo Jumatatu Juni 1, 2026, Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe amesema kati ya wanafunzi hao 172,114 sawa na asilimia 69.9 wamechaguliwa kujiunga katika shule za kutwa na bweni.

“Watakaojiunga shule za bweni na kutwa kidato cha tano ni wasichana 85,987 na wavulana 86,127 wenye sifa wamepangiwa katika shule 856 zikiwemo bweni 825, kutwa 25 na kutwa na bweni sita,” amesema.

Ukilinganisha na mwaka jana waliopangiwa kujiunga kidato cha tano walikuwa 188,787 katika shule 812 pekee.

Profesa Shemdoe amesema wanafunzi 1,548 wakiwamo wasichana 762 na wavulana 786 wamepangwa katika shule za sekondari nane zinazopokea wanafunzi wenye ufaulu wa juu.

“Katika mchanganuo, wanafunzi 163,499 wakiwemo wasichana 81,746 na wavulana 81,753 wamepangwa katika shule za bweni, huku wanafunzi 7,067 wakiwemo wasichana 3,479 na wavulana 3,588 wakipangwa katika shule za kutwa,” amesema.

Kwa upande wa vyuo vya elimu ya ufundi, wanafunzi 74,083 sawa na asilimia 30.1 wakiwemo wasichana 28,115 na wavulana 45,968 wamechaguliwa kujiunga na vyuo hivyo.

Amesema wanafunzi 3,144 wakiwemo wasichana 1,170 na wavulana 1,974 wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika vyuo vinne vya elimu ya ufundi. 

Vyuo hivyo ni Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Chuo cha Maendeleo ya Maji (WMDI).

“Pia wanafunzi 2,330 wakiwemo wasichana 1,165 na wavulana 1,165 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya afya ngazi ya stashahada, huku wanafunzi 2,983 wakiwemo wasichana 1,368 na wavulana 1,615 wakichaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu vya ngazi ya stashahada,” amesema.

Katika hatua nyingine, wanafunzi 65,626 wakiwemo wasichana 24,412 na wavulana 41,214 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya kada nyingine.

Profesa Shemdoe amesema muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa kidato cha tano utaanza Julai 6, 2026 hivyo wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na hatua hiyo wanapaswa kuanza kuripoti shuleni kuanzia Julai 4, 2026 na siku ya mwisho ya kuripoti ikiwa Julai 31, 2026.

“Kwa wanafunzi waliopangwa kwenye vyuo vya elimu ya ufundi watapokea maelekezo ya namna ya kujiunga kutoka katika vyuo walivyopangwa,” amesema.

Amesema uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo katika shule, hivyo hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule kutokana na ukosefu wa nafasi.

“Kwa wale wazazi mnaotamani watoto wenu wasome katika zile shule nane bora, hakutakuwa na nafasi ya uhamisho kwa sababu kumejaa,” amesema.

Ametumia pia fursa hiyo kuwapongeza walimu, wazazi na walezi kwa juhudi walizozifanya katika malezi na ufundishaji zilizowezesha wanafunzi kufaulu vizuri, huku akiwaomba kuendelea kusimamia na kufuatilia maendeleo ya watoto wao.

“Pia nawapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi na ninawahimiza kuendelea kufanya bidii katika kujifunza ili muweze kufanikiwa kujiunga na mafunzo ya elimu ya juu baada ya kuhitimu hatua hiyo ya elimu,” amesema.

Profesa Shemdoe ametoa wito kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha azma ya kuwa na shule za sekondari za kidato cha tano katika kila tarafa inatekelezwa.

“Kutekelezwa kwa azma hii itawezesha wanafunzi wote wanaofaulu mtihani wa kidato cha nne kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *