Mbeya. Watu wanne wamefariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea eneo la Maji Mazuri katika barabara ya Mbeya – Chunya ikihusisha basi la kampuni ya Mwasote.

Hii ni ajali ya pili kutokea ndani ya wiki moja, ambapo awali ilitokea wilayani Mbarali Mei 30 iliyoua watatu na kujeruhi wanne ikihusisha magari mawili basi la kampuni ya ABC Upper Class na rori.

Akithibitisha kutokea ajali hiyo, Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema imetokea Mei 31, ambapo basi hilo lilikuwa  likitokea Mbeya kuelekea wilayani Chunya liliacha njia na kupinduka.

Amesema katika ajali hiyo watu wanne walifariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa. Kuzaga  amewataja walipoteza maisha kuwa ni Hamza (30) na Matrida Mwabanganya anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 35-40.

Aidha amesema watu 29 wamejeruhiwa ambapo 11 wamelazwa, huku 18 wakiwamo wanaume 17 na mwanamke mmoja wamepata huduma katika Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya na kuruhusiwa kuondoka.

“Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva Nehemia Sanga mkazi wa Uyole kushindwa kulimudu gari lake katika eneo lenye kona kali kisha kuacha njia, dereva huyo anaendelea kutibiwa chini ya ulinzi,” amesema Kuzaga.

Maofisa Usalama Barabarani wakiwa katika eneo basi la kampuni ya Mwasote lililopata ajali katika maeneo ya maji mazuri wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani humo linamshikilia Siwema Simfukwe mfungwa aliyetoroka gerezani Mei 13 akiwa anatumikia kifungo cha miaka 30 kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha kwa tuhuma za matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Taarifa ya Kamanda Kuzaga imeeleza kuwa baada ya kutoroka gerezani amefanya matukio ya unyang’anyi uvunjaji na ubakaji katika maeneo ya Iwambi jijini Mbeya, likiwamo tukio la Mei 15 alipovamia nyumba ya mwananchi mmoja na kutishia kuua mtoto wa familia hiyo.

“Miongoni mwa matukio aliyofanya ni la Mei 15 saa 2:30 usiku ambapo alivamia nyumba akiwa na silaha (panga) na kutishia kuua mtoto wa familia hiyo iwapo hawatatii amri yake, kisha kuwafunga kamba na kuwabaka mama na binti wa kazi na kupora simu mbili na fedha Sh400,000.

“Aidha Mei 22 huko Iwambi alivamia nyumba nyingine na kupora simu na fedha Sh300,000 zilizokuwa kwenye simu baada ya kumuamuru atoe nywila na kufanikiwa kuhamisha kiasi hicho,” imeeleza taarifa hiyo.

Imeeleza kuwa kufuatia matukio hayo, Jeshi la Polisi kupitia askari maalumu lilifanya msako na Mei 30 huko Chipaka wilayani Momba mkoani Songwe na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo.

“Mtuhumiwa alikutwa na silaha iliyotengenezwa kienyeji, panga, Shot Gun moja, akibainisha kuwa kitendo cha kukutwa na silaha hizo kilizua hasira kwa wananchi kuanza kumshambulia, lakini jitihada za askari zilifanikiwa kumuokoa na kumkimbiza Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *