Iran imelaani vikali shambulio la kikatili lililofanywa na polisi wa Uholanzi dhidi ya mke mjamzito wa mwanamume Mpalestina, ikitoa wito kwa serikali ya Uholanzi kuchunguza tukio hilo na kuwawajibisha waliohusika.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, ametoa ujumbe huo leo Jumatatu kuhusu video iliyosambazwa na televisheni ya Al Jazeera inayomuonyesha afisa wa polisi wa Uholanzi akimtupa chini kwa nguvu mwanamke mjamzito na kumburuta wakati wa kukamatwa kwa mumewe Mpalestina.

“Mwenendo huu ni wa kikatili na hauwezi kuhalalishwa kabisa. Hakuna kisingizio kwa polisi wa Uholanzi kumshambulia mwanamke mjamzito kwa mabavu kwa sababu tu alitaka kuwa kando ya mumewe MPALESTINI aliyekamatwa,” ameandika Baghaei.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amewasihi maafisa wa serikali ya Uholanzi kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu ukiukwaji huo wa wazi wa haki za binadamu na kuwawajibisha wahusika.

“Mamlaka za Uholanzi lazima zihakikishe uwajibikaji kamili kwa ukiukwaji huu wa wazi wa haki za binadamu. Matukio kama hayo yanaonyesha upendeleo wa kimfumo na ubaguzi ndani ya vyombo vya sheria,” amesisitiza Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.

Tukio hilo, lililotokea Mei 19 katika mji wa Zeist nchini Uholanzi, lilipata umaarufu wa umma mwishoni mwa juma baada ya video kuibuka mtandaoni zikionyesha afisa wa polisi akimvuta kwa nguvu mwanamke mjamzito, na kumuangusha chini.

Kwa mujibu wa ripoti ya Al Jazeera, mume wa mwanamke huyo alikamatwa baada ya kudaiwa kuharibu televisheni baada ya kupokea habari za kifo cha jamaa zake huko Gaza. Mwanamke huyo alisema mumewe alishirikiana kwa heshima na polisi na kwamba alizuiliwa kwa nguvu na kutupwa chini baada ya kuomba ruhusa ya kuandamana naye.

Ripoti ya Al Jazeera imesema kwamba mwanamke huyo alianza kujifungua mapema kutokana na mfadhaiko, na baadaye akajifungua mtoto wa kike kabla ya wakati.

Japokuwa mama na mtoto aliyezaliwa wameripoti kuwa salama, lakini tukio hilo limezua uchunguzi na maswali mapya kuhusu mienendo ya maafisa wa polisi waliohusika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *