Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen imelaani vikali hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuimarisha vikwazo dhidi ya harakati za ukombozi wa Palestina, Hamas na Jihad Islami, ikiitaja kuwa ni ishara ya utiifu kwa Uzayuni wa kimataifa.

Ikijibu hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuongeza vikwazo dhidi ya Hamas na Jihad Islami, taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen iliyotolewa mapema leo Jumatatu, imesisitiza kwamba msimamo huo unapingana na misimamo chanya ya baadhi ya nchi za Ulaya, ikiwemo Uhispania, ya kulaani mauaji ya kimbari yanayofanyika huko Gaza.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa msimamo huo pia unapingana na maandamano ya watu wengi katika baadhi ya nchi za Ulaya na ushiriki wa baadhi ya wanaharakati kutoka nchi hizo katika msafara wa kimataifa wa “Global Sumud Flotilla” ili kuvunja kuzingirwa kwa Gaza.

Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen imesisitiza kwamba uamuzi wa Umoja wa Ulaya unaonyesha utiifu wake kwa Uzayuni wa kimataifa na ushawishi mkubwa wa Uzayuni katika nchi kadhaa za Ulaya, na imetoa wito kwa watu wa Ulaya kuwa macho na kuziwajibisha serikali zao kwa sera hizi za uadui.

Taarifa hiyo imesema: “Yemen, kwa mara nyingine inasisitiza uungaji mkono wake thabiti kwa watu wa Palestina, Hamas, Jihad Islami na makundi mengine ya muqawama na mapambano, na inasisitiza kuwa misimamo kama hiyo haitadhoofisha azma ya watu wa Palestina ya kupigania haki zao halali. Imesema Yemen itaendelea kuwa bega kwa bega na watu wa Palestina na makundi ya ukombozi kwa uwezo na rasilimali zake zote.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *