Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya unapasa kuzingatia kanuni ya utawala wa sheria na Hati ya Umoja wa Mataifa ambazo unadai kufungamana nazo.

Esmail Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amejibu taarifa ya Msemaji wa Umoja wa Ulaya inayokosoa hatua za Iran katika kujilinda dhidi ya mashambulizi ya kichokozi ya Marekani na utawala ghasibu wa Israel, na kusema: Umoja huo unapaswa kuheshimu kanuni ya utawala wa sheria na Hati ya Umoja wa Mataifa, ambazo umekuwa ukidai kuzilinda wakati wote, na kujiepusha na siasa za kumfurahisha mchokozi na kukemea pande zinazojitetea dhidi ya wachokozi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa: Tamko la Umoja wa Ulaya la kuilaani Iran kwa kutumia haki yake halali ya kujilinda dhidi ya mashambulio haramu ya Marekani kutokea moja ya nchi jirani kusini mwa Ghuba ya Uajemi, ni mfano wa wazi wa unafiki, siasa za undumakuwili na kutowajibika kisheria.

Amesisitiza kuwa hatua ya Iran ya kulenga vituo na suhula zinazotumika kwa ajili ya uchokozi wa kijeshi dhidi ya Iran ni hatua ya kisheria inayotekelezwa katika fremu ya haki ya kujilinda. Ameongeza kuwa: “Mataifa yana wajibu wa kisheria wa kuzuia wavamizi kutumia ardhi na suhula zao kushambulia nchi nyingine.”

Katika taarifa yake, Umoja wa Ulaya umelaani jibu madhubuti la Iran mkabala wa uchokozi uliofanywa hivi karibuni na Marekani kutokea Kuwait na kuzitaka pande zote eti ziheshimu kikamilifu sheria za kimataifa. Taarifa hiyo imedai kwamba Umoja wa Ulaya utaendelea kuunga mkono juhudi zote za kupunguza mivutano na kuunga mkono utatuzi wa kudumu wa vita kati ya Marekani, utawala wa Kizayuni na Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *