Jürgen Todenhofer, mwanasiasa na mjumbe wa zamani wa bunge la Ujerumani, amesema: “Umoja wa Ulaya na serikali ya Ujerumani zinahusika moja kwa moja katika maangamizi makubwa ya watu wa Palestina.”

Todenhofer anauchukulia Umoja wa Ulaya kuwa mshirika wa “ugaidi wa kimfumo” wa walowezi wa Israel katika hali ambayo ushahidi zaidi unachapishwa kila siku kuhusu kuongezeka ghasia na vitendo vya mabavu vya Walowezi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina huko Gaza, Ukingo wa Magharibi na Quds Mashariki (Jerusalem). Vurugu ambazo, licha ya kulaaniwa kwa maneno, zinaendelea bila kufungamana na gharama zozote za kisiasa kwa wahusika wake. Waangalizi wengi wa kimataifa wanazungumzia mradi ambao unalenga kubadilisha hatua kwa hatua jiografia na idadi ya watu wa Palestina. Mauaji ya halaiki ya Wapalestina baada ya Oktoba 2023 ni sehemu moja tu ya mradi huu wa kigaidi. Katika hali ambayo Ukanda wa Gaza umegeuzwa kuwa ardhi iliyoteketezwa, Ukingo wa Magharibi pia umeshuhudia ongezeko kubwa la mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni wenye itikadi kali, unyakuzi wa ardhi, ubomoaji wa nyumba na vizingiti chungu nzima katika maisha ya Wapalestina. Kwa kuzingatia hali hiyo, taarifa ya Todenhofer imepewa umuhimu maalum. Tofauti na walivyo wanasiasa wengi wa Ulaya, haelekezi kidole cha lawama kwa Tel Aviv pekee, bali pia anaangazia nafasi ya serikali za Magharibi katika kuendeleza jinai hii.

Kwa maoni yake, suala si vitendo vya walowezi au serikali ya Benjamin Netanyahu tu, bali pia ni kimya na kutochukua hatua serikali zinazodai kuwa wabeba bendera ya kutetea haki za binadamu na utekelezaji wa sheria za kimataifa ulimwenguni.

Ukweli ni kwamba Umoja wa Ulaya hauna misimamo ya wazi ya kisheria na kisiasa kuhusu ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina. Umoja huo umekuwa ukisema mara kwa mara kuwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina ni kinyume cha sheria na kwamba vinapingana na utatuzi wa serikali mbili. Umoja wa Mataifa pia umesisitiza msimamo huo huo katika makumi ya maazimio yake. Hata hivyo, swali la msingi hapa ni je: ikiwa ujenzi wa vitongoji ni kinyume cha sheria, basi kwa nini mchakato wa upanuzi wake haujasimamishwa?

Ikiwa unyanyasaji dhidi ya raia wa Palestina unalaaniwa na kukemewa kimataifa, kwa nini hakuna hatua zozote zinachukuliwa kwa ajili ya kuuzuia? Jibu la maswali haya linapaswa kutafutwa katika undumakuwili uliopo kati ya maneno na vitendo vya Umoja wa Ulaya katika uwanja huo. Umoja huo umetumia vikwazo, mashinikizo ya kiuchumi, na hatua za kutenga kisiasa katika kukabiliana na migogoro mingi ya kimataifa. Lakini kuhusu suala la Palestina, imetosheka tu na kutoa taarifa tupu za kidiplomasia katika kulaani jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia. Matokeo ya mbinu hii ni kwamba Tel Aviv imeepushwa kulipa gharama za kisiasa kutokana na sera zake za kigaidi na kibaguzi, jambo ambalo limeupelekea kuwa na kiburi zaid na kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kupora ardhi za Wapalestina kwa kasi kubwa zaidi.

Hali hii inaweka wazi zaidi “vipimo vya aina mbili” au undumakuwili unaotumika kwa madhara ya Wapalestina kuliko huko nyuma. Katika vita vya Ukraine, Ulaya imetumia uwezo wake wote wa kisiasa na kiuchumi kukabiliana na Mashambulizi ya Russia, kwa kisingizio cha kutekeleza sheria za kimataifa. Pamoja na hayo, lakini la kusikitisha ni kuwa kisingizio hicho hicho hakitumiki kuhusiana na ukaliwaji mabavu wa ardhi za Wapalestina na ujenzi haramu wa vitongoji vya Wazayuni. Ni mkanganyiko huo ndio unatilia shaka uaminifu wa kimaadili wa nchi za Magharibi mbele ya fikra za waliowengi duniani, haswa katika Asia Magharibi na Kusini mwa dunia.

Matokeo muhimu zaidi ya vipimo viwili hivi tofauti vya Ulaya kuhusu Palestina ni kumomonyoka taratibu kwa nguvu yake laini na kisheria katika utatuzi wa migogoro ya kimataifa. Katika miongo mitatu iliyopita, Umoja wa Ulaya umejaribu kujidhihirisha sio kama nguvu ya kijeshi, bali kama “nguvu ya kawaida” katika utatuzi wa migogoro; muigizaji anayepata uhalali na ushawishi wake kutokana na kutetea haki za binadamu, demokrasia, sheria za kimataifa na ushirikiano wa pande nyingi. Lakini vita vya Gaza na kimya cha Ulaya mkabala wa upanuzi wa vitongoji, mzingiro, kulazimishwa Wapalestina kuwa wakimbizi na mauaji ya umati dhidi ya raia vimetia doa madai hayo ya Ulaya.

Ulaya leo inakabiliwa na mgogoro wa uaminifu wa maadili na nguvu laini. Wakati inapochukulia uvamizi wa Ukrain kuwa ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kwa upande wa pili kukaa kimya mbele ya uvamizi wa miaka mingi wa ardhi za Palestina, watu katika nchi za Magharibi na duniani kote wanajiuliza swali kuwa je, sheria za kimataifa zinapaswa kutekelezwa kwa usawa kwa wote, au zinapaswa kutekelezwa tu kama chombo cha kisiasa kwa ajili ya kufikia malengo maalum katika pembe tofauti za dunia? Matokeo ya mbinu hii ya kibaguzi yanaonekana wazi katika kupungua ushawishi wa kisiasa na kimaadili wa Ulaya barani Afrika, Amerika ya Kusini na Asia. Katika mengi ya maeneo haya, maoni ya umma hayaichukulii tena Ulaya kama mpatanishi asiye na upendeleo au mtetezi wa haki za binadamu, bali kama sehemu ya muundo wa nguvu ambao umesalia kimya mbele ya mateso ya Wapalestina. Kwa sababu hiyo, vita vya Gaza si mgogoro kwa Wapalestina tu; bali pia ni mgogoro kwa hadhi ya kimataifa ya Ulaya. Kadiri pengo linavyozidi kuwa kubwa kati ya matamshi na vitendo vya Ulaya kuhusu haki za binadamu kuhusiana na Palestina, ndivyo nguvu ya ushawishi ya umoja huo, ushawishi wa kidiplomasia na nafasi yake katika mfumo wa kimataifa vinavyozidi kudhoofika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *