
TANGA: Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Tanga, Rajab Abdulrahman amekabidhi Sh milioni 500 kwa ajili ya umaliziaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba 36 za watumishi wa chama hicho ndani ya wilaya tisa za mkoa huo.
Akikabidhi Hundi ya fedha hizo kwa Katibu wa Chama hicho, Mfaume Kizigo hapo jana, Mwenyekiti Rajab alisema kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba mwaka huu huku akiongeza kuwa hatua inayolenga kuimarisha miundombinu na utendaji wa watumishi wa chama.
“Mradi huu unagharimu jumla ya Sh bilioni 2.5 fedha hizo zimepatikana kupitia michango mbalimbali, ikiwemo Sh milioni 56 zilizotolewa awali, milioni 10 zilizotolewa na MNEC sambamba na michango iliyokusanywa kutoka katika wilaya zote,”alisema.
Aidha, Mwenyekiti Rajab alisisitiza kuwa fedha zote zimeshapatikana, na kazi ya ujenzi imeshaanza kwa lengo la kuhakikisha malengo ya chama yanafikiwa ndani ya muda uliopangwa.
Alisema kuwa ujenzi wa chama ni mchakato endelevu usiokuwa na mwisho, akilinganisha na ujenzi wa miradi mingine ya kijamii kama shule, hospitali, na miundombinu ya barabara na reli.
Hivyo alitoa wito kwa wana-CCM wa mkoa wa Tanga kujitolea kwa nguvu zao, elimu, na fedha zao ili kukijenga chama kwa pamoja kwani uongozi wa chama hubadilika, lakini dhamira ya kuimarisha chama inapaswa kubaki thabiti, huku akisisitiza kuwa umoja na ushirikiano ndio nguzo kuu ya mafanikio ya chama hicho mkoani Tanga.
Kwa upande wake Katibu wa CCM mkoa wa Tanga Mfaume Kizigo alibainisha kuwa ujenzi wa nyumba hizi ni sehemu ya mikakati ya chama kukikamilisha na kukiongezea nguvu chama hicho katika ngazi ya wilaya.
“Kila wilaya imepangiwa kujenga nyumba nne, ambazo ni:Nyumba ya Katibu wa CCM wa wilaya,Nyumba ya Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa wilaya, Nyumba ya Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa wilaya na Nyumba ya Katibu wa Jumuiya ya UWT wa wilaya”alisema Kizigo