
Wizara ya Sheria ya Ufaransa imetangaza kwamba idadi ya wafungwa nchini humo imefikia zaidi ya watu 88,600, ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika historia ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Sheria ya Ufaransa, uwezo wa magereza za nchi hiyo haujaongezeka kulingana na ongezeko la idadi ya wafungwa, na msongamano katika baadhi ya magereza na vituo vya kizuizini umezidi asilimia 200.
Wakati huo huo, Inspekta Jenerali wa Magereza ya Ufaransa katika ripoti yake ya kila mwaka ameitaja hali katika magereza nchini humo kuwa “ya kutisha, ya kuaibisha na ya majanga”, akionya kuhusu msongamano wa watu, hali duni ya usafi na ongezeko la vurugu na machafuko.
Mashirika ya ndani na ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakikosoa hali ya magereza ya Ufaransa kutokana na changamoto kubwa za haki za binadamu, hasa kutokana na msongamano wa watu, hali zisizo za kibinadamu na ukosefu wa suhula za afya ya mwili na afya ya akili.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la HRW pia katika ripoti yenye kichwa cha habari “Adhabu Maradufu” limeashiria ukosefu wa wataalamu wa afya ya akili katika magereza ya Ufaransa na kusisitiza kwamba msongamano na kutengwa vinazidisha hali mbaya za wafungwa wenye ulemavu wa akili.
Ripoti hiyo inasema, kiwango cha kujiua katika magereza ya Ufaransa ni mara saba zaidi ya idadi ya watu kwa ujumla, na zaidi ya 25% ya wafungwa wanakabiliwa na matatizo ya akili, huku uchunguzi na wanasaikolojia ukiwa nadra na kwamba unaishia kwenye kuagiza dawa tu.