
Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamehoji usalama wa Taifa na taarifa za Serikali kutokana na matumizi ya mifumo ambayo inaundwa na inamilikiwa na kampuni kutoka mataifa mengine.
Hayo yamebanishwa leo Juni mosi, 2026 wakati wakijadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Barazani Chukwani, Unguja Zanzibar.
Akichangia bajeti hiyo, mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayub (CCM) amesema mifumo ya Serikali inasimamiwa nje ya nchi akihoji usalama wa taarifa za Serikali na usalama wa Taifa kwa ujumla wake.
“Watengenezaji wa mifumo hii wapo nje ya nchi, Hii mifumo unakuta ipo nje, tunajua Serikali na usalama wake lakini unatoka wapi wakati mifumo ipo nje, umefika wakati sasa kuwa na mifumo yetu hapa,” amesema Ayub.
Hoja hiyo pia imechangiwa na mwakilishi wa Ole Seif Hamad Suleiman ambaye amesema amehoji kwa nini Serikali isiwe na mifumo yake yenyewe.
Pia Seif amezungumzia kuhusu intaneti akisema inasumbua na katika mipango ya Serikali ya kuleta ubunifu haiwezi kufanikiwa ikiwa hakuna intaneti imara.
Seif amesema, “kuna shida ya mifumo ya Serikali kutosomana kila ofisi unayokwenda unahitaji kuweka taarifa upya, tuelezwe hapa kuna mpango gani kuhakikisha mifumo ya taasisi inasomana.”
“Ukienda kuangalia taarifa za vizazi na vifo unakuta taarifa hazielewani, hii inatokana na mifumo kutooana kama ingekuwa inaoana huwezi kukuta changamoto hiyo.
Pia mwakilishi nafasi za wanawake Aza Januari Joseph (CCM) amesema kutosomana kwa mifumo inakuwa kero kwa wananchi huku kuundwa mifumo na wataalamu wa nje kunaibua wasiwasi na usalama na kutumia gharama kubwa inapopata changamoto.
Mwakilishi wa Magomeni, Mahfoudh Abdala Mohamed amesema iwapo sekta hiyo ikishughulikiwa vizuri italeta matokeo kwani kuna bunifu nyingi ila zinakufa.
Mapema akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, Waziri Mudrik Ramadhan Soraga ameomba baraza kuidhinisha Sh53.391 bilioni kutekeleza vipaumbele vinne.
Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni mazingira wezeshi kwa kutunga, kuhuisha na kusimamia utekelezaji wa Sera ya kidijitali ya Zanzibar ya mwaka 2026 na kuendelea na hatua za kuandaa rasimu ya sheria ya Kampuni Chipukizi na Ubunifu.
“Kutunga sheria ya Tehama na kukamilisha hatua za kuandaa rasimu ya sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.
Kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza na kuimarisha anuani ya makaazi: kwa kuendelea kutoa, kusajili na kuzihakiki, kuendeleza matumizi ya mfumo huo katika utoaji wa huduma kidjitali pamoja na kutoa elimu na uelewa wa mfumo.
Kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuchochea ubunifu na kuimarisha ustawi wa kampuni chipukizi kwa kuendelea kutoa mafunzo ya Tehama na elimu ya dijitali kwa wananchi kupitia Vituo vya Tehama jamii, pamoja na kuendelea na ujenzi wa kituo cha ubunifu na ujasiriamali.
“Kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote na kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano kwa kujenga minara ya mawasiliano katika maeneo yenye changamoto za upatikanaji wa huduma ya mawasiliano Unguja na Pemba,” amesema.
Maoni ya Kamati
Kamati ya miundombinu, Ardhi na Tehama imesema licha ya maono mazuri ya Serikali ya kuanzisha wizara hii, kamati inaona ipo haja kwa Wizara ya Fedha kuyaangalia vizuri makadirio ya matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwani ni ndogo ikilinganishwa na uhalisia wa utekelezaji wa huduma zinazotarajiwa kutolewa.
Akisoma maoni ya kamati hiyo Makamu Mwenyekiti, Mwanaidi Kassim Mussa amesema Ikiwa katika hatua za kuanzishwa kwake, Wizara hiyo inahitaji uwekezaji mkubwa wa kifedha ili iweze kuzihudumia wizara nyingine zote katika nyanja za mawasiliano, Tehama na ubunifu.