Dodoma. Serikali imesema kuwa, licha ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa vipaumbele kwa Wizara ya Fedha katika bajeti ya 2025/26, zipo changamoto zilizojitokeza pia.

Miongoni mwa changamoto hizo n kuongezeka kwa gharama za mikopo katika masoko ya fedha ya nje na hivyo kuathiri upatikanaji wa kiwango cha mikopo iliyotarajiwa.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamisi Mussa Omar ametaja changamoto hizo leo Jumanne Juni 2,2026 wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Katika bajeti hiyo, Wizara imeomba kuidhinishiwa Sh21.3 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya wizara na taasisi zake.

Waziri ametaja changamoto nyingine ni mwitikio mdogo wa matumizi ya teknolojia

na mifumo ya kielektroniki ya malipo, hivyo kuathiri ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, kuongezeka kwa migogoro ya biashara,   gharama za kupata bidhaa na huduma mbalimbali na  kubadilika kwa sera za washirika wa

maendeleo na kusababisha kupungua kwa misaada katika maoteo ya mwaka 2026/27.

Nyingine ni kiwango kikubwa cha malimbikizo ya madeni na madai ya makandarasi, watoa huduma na wazabuni na kuongezeka kwa mahitaji ya kujenga uwezo kwa watumishi wa umma kuhusu uzingatiaji wa masuala ya mazingira na matumizi ya Akili Unde (AI).

“Ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeza, Wizara imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha mifumo na kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani,” amesema Balozi Khamisi.

Baadhi ya mikakati aliyoitaja ni kuongeza kiwango cha ukopaji kutoka soko la ndani la fedha kufuatia mwenendo mzuri wa minada ya hatifungani za Serikali na kampuni.

Mikakati mingine ni pamoja na kuhamasisha na kuimarisha matumizi

ya mifumo ya kielektroniki katika malipo, utoaji huduma, ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa fedha za umma.

“Tutaboresha mazingira ya uwekezaji, biashara na urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ili kuongeza wigo wa mapato ya

ndani, kutenga bajeti kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya madeni na madai ya makandarasi, watoa huduma na wazabuni na kutenga bajeti kwa ajili ya kujenga

uwezo kwa watumishi,”amesema.

Amesema watafanya kazi ya kujenga uwezo wa watumishi ili kuwa na  uzingatiaji wa masuala ya mazingira na matumizi ya Akili Unde (AI) katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *