
Babati. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Watanzania kuendelea kudumisha mshikamano wa kitaifa na kukataa kwa nguvu zote vitendo vinavyoweza kuligawa taifa, vikiwemo udini, ukabila na ukanda.
Chama hicho kimesema vitendo hivyo havina nafasi katika jamii ya Kitanzania, kikisisitiza kuwa msingi wa taifa hili umejengwa katika umoja, usawa na kuheshimiana tangu uhuru.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Juni 2, 2026 na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Ayalagaya, Kata ya Dareda, wilayani Babati mkoani Manyara, katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua uhai wa chama, utekelezaji wa ilani na miradi ya maendeleo.
Kihongosi amesema Watanzania wanapaswa kuunganishwa zaidi na utaifa wao, utu na mapenzi kwa nchi yao badala ya kugawanywa na tofauti za kikabila, kidini au kikanda.
“Nchi tunayoitaka ni ile isiyobagua watu. Tunapoyaona mambo ya kuhamasisha ubaguzi kwa misingi ya dini, ukabila au ukanda, ni lazima tuyakatae kwa sababu yanaweza kuligawa taifa letu. Tujenge mshikamano wa Utanzania wetu,” amesema.
Amesisitiza kuwa misingi ya taifa imejengwa juu ya amani na usawa, akiwataka wananchi kuishi kwa upendo na kuheshimiana bila kujali tofauti zao.
Kihongosi amemtaja Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kama kielelezo cha msisitizo wa umoja wa kitaifa, akisema dira yake bado inaendelea kuwa nguzo muhimu ya mshikamano nchini.
“Tanzania yetu haigawanyiki. Hapa ni kwenu, na kila Mtanzania ana haki ya kuishi na kufanya kazi popote nchini bila kubaguliwa kwa misingi ya dini, kabila au eneo analotoka,” amesema.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo alipuuzia madai ya baadhi ya watu wanaosema hakuna maendeleo yaliyofanywa na CCM, akisema miradi mikubwa ya kimkakati inaonyesha wazi mabadiliko makubwa yaliyopatikana nchini.
Alitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Reli ya Kisasa (SGR) na Daraja la Kigongo-Busisi, akisema yote imekamilika na sasa wananchi wananufaika nayo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Bila aibu kuna wanaosema hawaoni kitu CCM inafanya. Tanzania ya mwaka 1961 inafanana na ya leo? Maendeleo yapo wazi katika kila sekta,” amesema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kupinga upotoshaji kwa kutoa taarifa sahihi kwa wananchi, akisema ni wajibu wa kila mtu kulinda ukweli kuhusu maendeleo ya nchi.
Awali, alipokuwa akitembelea Shule ya Sekondari Beselo, Kihongosi aliagiza TANESCO na mamlaka za maji kuongeza kasi ya kutatua changamoto za umeme na maji katika shule na vijiji, akisisitiza kuwa huduma hizo ni msingi wa maendeleo.
Kwa upande wake, mmoja wa wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo, Leonard Gwandu, alisema ujenzi wa shule hiyo mpya ulifanyika kwa ushirikiano kati ya wazazi na serikali ili kupunguza msongamano uliokuwepo katika Shule ya Sekondari Dareda.