Dar es Salaam. Kilimo kinaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, kikichangia takribani asilimia 26 ya pato la Taifa na kuajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania.
Ukuaji huu unaifanya sekta hiyo kubaki kitovu cha fursa za uwekezaji na mtaji, hasa katika mnyororo wa thamani wa mazao.
Katika majadiliano ya wadau katika Jukwaa la Uwekezaji wenye athari chanya (TIIF) jijini Dar es Salaam, unaofanyika leo Jumanne Juni 2, 2026, Luiana Temba, Mkurugenzi wa Shirika la Ushauri wa Maendeleo ya Biashara kutoka Kenya, amesema sekta za kilimo, uchumi wa buluu, teknolojia na mazao ya misitu ndizo zinazoibeba Tanzania katika kuvutia mitaji ya uwekezaji.
Ameweka wazi kuwa kilimo cha mazao, uvuvi, na asali ni sekta zinazoendelea kukua na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Hata hivyo, licha ya kuwa na fursa kubwa za faida na ukuaji, amesema bado zinakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mitaji na miundombinu ya uwekezaji, hali inayowafanya wafanyabiashara wengi kushindwa kunufaika kikamilifu.
“Takwimu zinaonyesha kuwa kuna pengo la ufadhili linalokadiriwa kufikia takribani Sh861 trilioni kwa biashara ndogo na za kati (SMEs) katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, hali inayoonyesha kuwa sekta zenye fursa kubwa za uwekezaji bado hazipati mtaji unaolingana na mahitaji yake,” amesema.
Ameongeza kuwa karibu asilimia 40 ya biashara hizo katika sekta hizi zinakabiliwa na ukosefu wa fedha kama kikwazo kikuu cha kukua na kuvutia wawekezaji, huku Afrika ikiwa na kiwango kidogo cha uwekezaji wenye athari chanya duniani cha takribani asilimia 12 tu.
“Hii inaonyesha wazi kuwa sekta zenye fursa kubwa za uwekezaji zinahitaji mifumo mipya ya ufadhili ili kuvutia mtaji zaidi na kuongeza athari za kijamii na kiuchumi,” amesema.
Wafanyabiashara waeleza uhalisia
Kwa upande wa wafanyabiashara nchini, Judith Masika, Mtaalamu wa nyaraka za usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi wa kampuni ya Megnacio nchini Tanzania, amesema sekta ya kilimo imeanza kuingia kwa nguvu katika masoko ya kimataifa kupitia majukwaa ya uwekezaji ikifungua milango ya mitaji na masoko mapya.
“Sekta ya kilimo sasa imekuwa daraja la fursa za uwekezaji wa kimataifa. Kupitia majukwaa haya tunakutana na wanunuzi na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali, jambo linalofungua soko kubwa la bidhaa zetu,” amesema.
Wafanyabiashara wakishiriki katika ukwaa la Uwekezaji wenye athari chanya (TIIF) jijini Dar es Salaam, Jumanne June 2, 2026.
Ameongeza kuwa kampuni yake inayojihusisha na mazao ya kahawa, korosho, kakao na ufuta, imefanikiwa kuvutia masoko ya nje tangu mwaka 2012, na sasa bidhaa za Tanzania zinapata nafasi kubwa katika masoko ya nje.
“Bidhaa zetu zinapendwa sana huko nje hasa Uturuki, Uholanzi, Dubai na Vietnam,” amefichua.
Naye Irene Ivambi, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mrembo Naturals, amesema sekta ya uchakataji wa mazao ya kilimo ni eneo kubwa la fursa za uwekezaji ambalo linavutia wadau wengi ingawa bado halijatumika kikamilifu.
Amesema ongezeko la mahitaji ya bidhaa za kilimo duniani limeifanya sekta hiyo kuwa kivutio kikubwa cha mitaji, ambapo kampuni yake imekua zaidi ya mara 20 kutokana na kuongezeka kwa masoko ya nje.
Hata hivyo, ameweka wazi kuwa changamoto kubwa bado ni upotevu wa mazao na ukosefu wa uwekezaji wa kutosha katika teknolojia ya uchakataji.
“Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 40 ya mazao ya kilimo hupotea kila mwaka baada ya kuvunwa katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, hali inayopunguza mvuto wa sekta hiyo kwa wawekezaji. Aidha, asilimia 96 ya mazao nchini Tanzania huuzwa bila kuongeza thamani, jambo linalopunguza fursa za faida kwa wawekezaji na wazalishaji,” amefafanua.
Amesema hatua hiyo inafanya Tanzania kuendelea kuagiza bidhaa zilizoongezwa thamani kutoka nje, licha ya kuwa na malighafi za kutosha ndani.
“Soko la dunia la bidhaa za kilimo linakua kwa wastani wa asilimia 10.5 kila mwaka. Hali hii inaonyesha sekta hii ina nafasi kubwa ya kuvutia mitaji ya viwanda vya uchakataji na kuongeza thamani,” ameongeza.
Kwa upande wa teknolojia, Antonio Lazaro wa kampuni ya Ikale, inayojihusisha na urejereshaji wa plastiki amesema sekta ya urejelezaji wa plastiki ni mfano wa sekta zinazoibuka na kuvutia mitaji kutokana na faida zake za kiuchumi na kimazingira.
“Kwa kipindi cha mwaka jana tumeweza kuchakata zaidi ya tani 5,000 za plastiki na mpaka sasa tumezalisha zaidi ya ajira 1,000, jambo linaloonyesha uwezo wa sekta hii kuwa eneo la kuvutia uwekezaji mkubwa,” amesema.
Akifafanua kuhusu mwenendo wa uwekezaji nchini, Alley Breedlove, Meneja wa Taasisi ya Third Partners, amesema mfumo wa ufadhili nchini unaonyesha mwelekeo katika eneo hilo kujikita kwenye uwekezaji wa umiliki wa sehemu ya biashara (hisa) huku taasisi za kifedha zikionekana kutokidhi mahitaji yaliyopo, hatua inayofanya biashara nyingi kuishia njiani.
“Takwimu za mwaka 2020 hadi 2025 zinaonesha kuwa misaada ya kifedha ilihusisha miradi 59 yenye thamani ya takribani Sh87 bilioni, uwekezaji wa umiliki wa biashara ukiwa na miradi 38 yenye thamani ya takribani Sh597 bilioni huku mikopo ikiwa na miradi saba pekee yenye thamani ya Sh28 bilioni,” amesema.
Ameeleza kuwa mwelekeo wa sasa wa mitaji nchini Tanzania unaelekezwa zaidi kwenye sekta za kilimo na chakula, jambo linalothibitisha kuwa sekta hizi ndizo zinazoongoza katika kuvutia uwekezaji, lakini bado zinahitaji upanuzi wa vyanzo vya ufadhili ili kuongeza kasi ya ukuaji wa biashara nchini.