Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeliondoa rasmi mahakamani shauri la maombi lililokuwa limefunguliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, akiomba kuunganishwa katika kesi ya madai iliyokuwa inakikabili chama hicho.

Shauri hilo limeondolewa mahakamani hapo na Jaji David Ngunyale leo Jumanne Juni 2, 2026 baada ya kesi ya msingi ya madai ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama hicho baina ya Bara na Zanzibar na ubaguzi, ambayo Lissu alikuwa ameomba kuunganishwa kwayo kufutwa, Mei 28, 2026.

Hata hivyo, wakati shauri hilo la Lissu likiondolewa mahakamani kutokana na kufutwa kwa kesi ya msingi, waliokuwa wamefungua kesi hiyo wanaendelea na majadiliano kuhusu hatima ya kesi hiyo baada ya kufutwa kama wanaweza kurudi tena au la.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ilikuwa imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu (marehemu kwa sasa).

‎Wadaiwa katika kesi hiyo walikuwa ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Kutokana na kesi hiyo, Lissu alifungua shauri la maombi akiomba kujumuishwa katika kesi hiyo kwa wadhifa wake wa kiongozi mkuu wa chama hicho yaani Mwenyekiti wa Chadema Taifa pamoja na mambo mengine, akidai kuwa ana masilahi katika kesi hiyo.

Wajibu maombi wa kwanza mpaka wa tatu walikuwa ni wadai katika kesi ya msingi, yaani Mohamed, Khamis na Komu; na Bodi ya Wadhamini Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema (wajibu maombi wa nne na wa tano mtawalia) ambao ni wadaiwa katika kesi ya msingi.

Shauri hilo la maombi mchanganyiko namba 12194/2026 lilitajwa kwa mara ya kwanza mahakamani Mei 25, 2026 ambapo mahakama ilitoa amri kwa wadaawa kukamilisha taratibu za ubadilishaji nyaraka kisha ikapanga kusikiliza shauri hilo leo Juni 2, 2026.

Hata hivyo, usikilizwaji wa shauri hilo kwa tarehe hiyo ulikuwa unategemea uamuzi wa pingamizi la wadaiwa katika kesi ya msingi kuhusiana na uhalali wake wanaodai kuwa ni batili kwa kuwa imekiuka mastakwa ya kisheria kwa kutokubainisha muda wa kuanza kwa madai yao (mambo wanayoyalalamikia).

Jaji Ngumyale katika uamuzi wake alioutoa Mei 28, 2026, alikubaliana na pingamizi hilo na akaifuta kesi hiyo. Kwa uamuzi huo shauri la Lissu halikuwa na miguu tena ya kusimamia mahakamani.

Kama ambavyo mahakama ilikuwa imepanga kuwa tarehe ya usikilizaji wa shauri hilo, Lissu amefikishwa mahakamani hapo leo kwa ajili hiyo.

Wakati Lissu amefikishwa mahakamani amejikuta akiwa peke yake kwani mawakili wa wajibu maombi wote, kwa maana ya walikuwa walalamikaji katika kesi ya msingi na waliokuwa walalamikiwa (Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu) hawakuwepo.

Hata hivyo, kwa kuwa tayari kesi ya msingi imeshafutwa, Lissu amearifiwa tu na Jaji Ngunyale kuwa kutokana na uamuzi wa kesi ya msingi shauri hilo limeondolewa mahakamani.

Mei 28, baada ya uamuzi wa mahakama ulioifuta kesi ya msingi, kiongozi wa jopo la mawakili wa waliokuwa wadai Shabani Marijani alieleza kuwa wanasubiri maelekezo ya wateja wao kuona kama wataweza kufungua tena kesi hiyo baada ya kurekebisha kasoro zilizobainishwa na mahakama.

Leo, wakili Marijani amelieleza Mwananchi tayari wameshakutana na kukaa na wateja wao kujadili uamuzi huo na wanaendelea na majadiliano hayo.

“Kwa hiyo kwa sasa siwezi kusema kwa undani, lakini tukimaliza majadiliano tutakujulisha uamuzi tutakaoufikia,” amesema wakili Marijani.

‎Katika kesi ya msingi, wadai walikuwa wanadai kuwa  kumekuwa na  mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

‎Pia walikuwa wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo walikuwa wanaomba Mahakama hiyo itamke kuwa wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.

Pia walikuwa wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa  ni kinyume cha sheria na ni batili.

Vilevile walikuwa wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa, na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na gharama za kesi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *