NAHODHA wa Serengeti Girls, Elizabeth John amesema timu hiyo imeshindwa kufikia malengo waliyojiwekea ya kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 17 baada ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Afrika Kusini kwa mabao 2-0, matokeo ambayo yaliwaweka kwenye mazingira magumu ya kusonga mbele.

Serengeti Girls ilishuka dimbani juzi Mei 31 katika Uwanja wa Lucas Moripe, Afrika Kusini saa 10 jioni kwenye mechi ya marudiano na ikatoka suluhu baada ya kupoteza mechi ya kwanza nyumbani kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Akizungumza na Mwanaspoti Elizabeth amesema wachezaji walikuwa na matumaini makubwa ya kuandika historia nyingine kufuzu fainali hizo, lakini walijikuta wakishindwa kutumia vizuri faida ya kucheza nyumbani na kuruhusu wapinzani wao kupata ushindi uliobadili mwelekeo wa mchujo huo.

Alieleza maumivu makubwa kwa kikosi hicho ni kushindwa kuendeleza mafanikio yaliyowekwa na kizazi cha Serengeti Girls kilichoshiriki Kombe la Dunia mwaka 2022 India na kufika hatua ya robo fainali, jambo lililowapa hamasa kubwa kabla ya kuanza kampeni za mwaka huu.

“Malengo yetu yalikuwa makubwa. Tulitaka kufuzu Kombe la Dunia na kuendeleza yale yaliyofanywa na dada zetu mwaka 2022, lakini kwa bahati mbaya hatukuweza kufanikisha hilo,” amesema Elizabeth.

Nahodha huyo amesema licha ya matokeo hayo, kikosi hicho kimejifunza mambo mengi katika safari ya mchujo na anaamini uzoefu walioupata umewapa somo kubwa.

Tanzania imeondolewa raundi ya pili kwa jumla ya mabao 2-0 dhidi ya Afrika Kusini, safari yao ilianzia raundi ya kwanza baada ya kuiondosha Botswana kwa jumla ya mabao 6-2.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *