Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewataka wadau wa kahawa mkoani humo kuhakikisha kuwa uzalishaji wa zao hilo unaenda sambamba na upatikanaji wa masoko ya uhakika ili kuwawezesha wakulima kunufaika zaidi na zao hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 30, mwaka huu  na Mkuu wa huo, katika taarifa yake  iliyosomwa  na Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi, Shaban Mchomvu  katika mkutano wa wadau wa kahawa Kanda ya Kaskazini ambao umewakutanisha mjini Moshi kujadili masuala mbalimbali yanayololikabili zao hilo la kahawa katika ukanda huo.

Aidha, amesema kuwa uzalishaji wa kahawa ni lazima uendane na upatikanaji wa masoko ya uhakika, huku akisisitiza umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya kahawa na bidhaa zake katika soko la ndani ili kuongeza thamani na manufaa kwa wadau wa zao hilo.

“Uzalishaji wa kahawa lazima uendane na upatikanaji wa masoko ya uhakika. Mafanikio ya zao lolote yanategemea uwepo wa tafiti za kina zinazowezesha upatikanaji wa mbegu bora na miche bora, jambo ambalo ni muhimu katika kuongeza tija na ubora wa kahawa,” amesema.

Amesema, “Ni muhimu kwa wataalamu wa utafiti pamoja na wale waliopo katika halmashauri zetu kushiriki kikamilifu katika suala hili kwa kubuni na kusimamia mbinu mbalimbali za kulinda na kuboresha kahawa kuanzia shambani hadi kufika sokoni, ili kuhakikisha inafuata viwango na taratibu zinazotakiwa.”

Amesema katika jitihada za kuimarisha bei ya kahawa, lazima kuwepo na juhudi mbalimbali za kuhakikisha ubora wa zao hilo unaongezeka na kuendeleza jina la kahawa ya Kilimanjaro katika masoko ya ndani na ya Kimataifa.

“Ongezeko la uzalishaji linapaswa kwenda sambamba na mikakati ya kuimarisha sekta hii ya kahawa kila mmoja akitambua umuhimu wa zao la kahawa kwa maendeleo ya mkoa wetu kwa ujumla,” amesema

Akizungumza katika mkutano huo, Ofisa Masoko Mwandamizi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Naishok Lukumay, amesema taasisi hiyo imeendelea kuhamasisha matumizi ya mbegu bora za kahawa kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa zao hilo, kwa kuzingatia viwango vinavyohitajika katika masoko ya kimataifa.

“Zao hili la kahawa halihitaji nguvu nyingi, hivyo kupitia Kituo cha utafiti wa kahawa (TaCRI)tumekuja na mbegu bora inayoitwa Compact.Mbegu hii inastahimili ukame, magonjwa na sio kama ile mbegu ya mwanzo ambayo inahitaji dawa nyingi na mvua nyingi au kumwagilia hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi,”amesema  Naishok

Aidha, amewataka wazee wa mkoa huo kuwahamasisha vijana kujihusisha na kilimo hicho cha kahawa ili kurejesha hadhi ya zao hilo mkoani humo.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji wa kahawa na kuwawezesha vijana kuinua vipato vyao kupitia fursa mbalimbali zinazopatikana katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Naye, Mshauri wa Kilimo huo, Godwin Maro, amesema mkoa huo umelenga kuzalisha tani 5,000 za kahawa katika msimu wa mwaka 2025/2026.

Maro amesema katika msimu wa mwaka 2024/2025, mkoa huo ulizalisha takriban tani 4,000 za kahawa, huku lengo la mwaka 2025/2026 likiwa ni kuzalisha zaidi ya tani 5,000 kupitia matumizi ya miche bora ya kahawa aina ya Compact inayozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI).

“Katika Mkoa wa Kilimanjaro, msimu wa mwaka 2024/2025 tuliweza kuzalisha takriban tani 4,000 za kahawa. Mwaka huu wa 2025/2026 tumelenga kuzalisha zaidi ya tani 5,000, na mkakati wetu ni kuendelea kupanda miche bora ya kahawa aina ya Compact kutoka TaCRI,” amesema Maro.

Amesema katika msimu uliopita, mkoa huo ulisambaza miche milioni 1.2 ya kahawa kwa wakulima, jambo lililochangia kuongezeka kwa hamasa ya uzalishaji wa zao hilo.

Aidha, amesema katika mwaka 2025/2026, Mkoa wa Kilimanjaro umesambaza miche milioni 1.4 ya kahawa, ambayo tayari imepokelewa na wakulima na inaendelea kupandwa katika mashamba mbalimbali.

Maro amesema miche hiyo huanza kuzaa baada ya miaka miwili hadi mitatu, na kwamba baada ya kipindi hicho uzalishaji wa kahawa katika Mkoa huo unatarajiwa kuongezeka maradufu ikilinganishwa na kiwango cha sasa.

“Baada ya miaka mitatu, uzalishaji wa kahawa katika Mkoa wa Kilimanjaro utaongezeka kwa kiasi kikubwa na tunaweza kufikia lengo la kuzalisha tani 10,000 kwa mwaka,” amesema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *