Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amemteua aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy  Mwalimu, kuwa Mshauri wa Rais katika masuala ya afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumanne, Juni 2, 2026 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, imeeleza kuwa Rais amefanya uteuzi huo leo.

Uteuzi huo unatajwa kuwa sehemu ya jitihada za kuimarisha zaidi sekta ya afya nchini, hususan katika maeneo ya afya ya uzazi na mtoto ambayo yameendelea kupewa kipaumbele na Serikali katika miaka ya hivi karibuni. Tanzania imekuwa ikipata mafanikio katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga kupitia uwekezaji mkubwa katika huduma za afya ya mama na mtoto.

Ummy Mwalimu ni mwanasiasa na mwanasheria mwenye uzoefu katika utumishi wa umma.

Katika maisha yake ya kisiasa, Ummy alianza kuwa Mbunge wa Viti Maalumu mwaka 2010 kabla ya kuendelea kushika nyadhifa mbalimbali serikalini.

Aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kati ya mwaka 2010 na 2014. Mwaka 2014 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mazingira.

Mwaka 2015, Rais wa awamu ya tano, hayati John  Magufuli, alimteua kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, nafasi aliyohudumu hadi mwaka 2020.

Baadaye alihamia Ofisi ya Makamu wa Rais kama Waziri wa Nchi anayeshughulikia Muungano na Mazingira kabla ya kupelekwa Ofisi ya Rais – Tamisemi mwaka 2021.

Mwaka 2022 alirejea Wizara ya Afya na kuendelea kuhudumu hadi mwaka 2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *