Kigoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma linawashikilia watu sita kwa kosa la kufanya vurugu na kuchoma moto lori la kubebea mchanga aina ya Howo, baada ya dereva wa gari hilo kumgonga na kumsababishia kifo mwendesha bodaboda.
Tukio hilo lilitokea Juni Mosi, 2026 katika Mtaa wa Mnarani, karibu na ofisi ya mabasi ya Adventure, Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambapo ilidaiwa kuwa bodaboda huyo aliingia chini ya uvungu wa lori hilo baada ya kugongana uso kwa uso wakati akimkwepa mwendesha baskeli,
Bodaboda aliyefariki katika ajali hiyo amefahamika kwa jina la Amir Masoud, maarufu ‘Pisi Kali’ anayedaiwa kuendesha katika upande usio wake.
Baadhi ya mashuhuda waliokuwa eneo la tukio walieleza kuwa baada ya ajali hiyo, bodaboda waliokuwa jirani na eneo hilo, kwa hasira walivamia lori hilo na kulichoma moto.
Lori hilo linafanya kazi ya kubeba madini katika mradi wa ujenzi tawi la Benki Kuu (BoT) Kigoma katika eneo hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 2, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu amesema dereva wa lori hilo alikimbia baada ya kusababisha ajali ili kuepuka hasira za bodaboda hao, hata hivyo alijisalimisha polisi.
“Hakuna majeruhi maana yule bodaboda aliyegongwa alifariki na dereva alikimbia, lakini alipatikana na hakudhurika, tunaendelea na upelelezi, tunaangalia ushahidi ukoje na ukikamilika tutawafikisha mahakamani,” amesema.
Katika harakati za kuwatawanya bodaboda hao, Jeshi la Polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwezesha Jeshi la Zimamoto kuendelea na shughuli ya uokozi.
Kamanda Makungu amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini mmiliki halali wa gari hilo.
Aidha, Kamanda Makungu amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi na badala yake kuviachia vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa matukio kama hayo.
“Ninawaomba sana wananchi hasa vijana kutojichukulia sheria mkononi, kama ajali imetokea taratibu za kisheria zipo wazi,” amesema.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma, Mrakibu Msaidizi Michael Maganga amesema jeshi hilo lilifika eneo la tukio baada ya kupokea taarifa na kuanza juhudi za kuzima moto uliokuwa umewashwa na wananchi.
Hata hivyo, Maganga amesema operesheni ya kuzima moto ilikumbana na upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya wananchi, ambao hawakutaka gari hilo liokolewe na wakitupa mawe dhidi ya askari wa Zimamoto waliokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Amir Masoud maarufu kwa jina la ‘Pisi kali’, Ofisa usafirishaji’bodaboda’ aliyefariki kwa kugongwa na Lori aina ya Howo eneo la mnarani mtaa wa Adventure, Manispaa ya Kigoma ujiji na kupelekea bodaboda wenye hasira Kali kuchoma moto gari lililosababisha ajali.
“Baada ya kuanza kuzima moto, wananchi walianza kutushambulia kwa mawe wakisema tusizime moto kwa sababu lori hilo limemgonga mwenzao, kwa hiyo imesababisha kuharibu gari letu, kioo cha mbele kimevunjwa vunjwa na wananchi,” amesema Kamanda Maganga.