Dodoma. Wizara ya Fedha imeweka wazi vipaumbele vinane vitakavyoongoza utekelezaji wa majukumu yake pamoja na taasisi zilizo chini yake, huku ikiomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh21.3 trilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma leo Jumanne Juni 2, 2026, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema Serikali inalenga kuendelea kusimamia uchumi kwa weledi ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi unafikia asilimia 6.3 mwaka 2026.

Amesema miongoni mwa malengo muhimu ni kudhibiti mfumuko wa bei ili ubaki katika kiwango cha wastani wa asilimia 3 hadi 5, pamoja na kuhakikisha akiba ya fedha za kigeni inatosheleza mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

Balozi Omar amesema Serikali pia itaendelea kuimarisha nidhamu ya usimamizi wa fedha za umma kwa kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato, ugawaji wa rasilimali, ununuzi wa umma na matumizi yenye thamani halisi ya fedha.

Pia, juhudi zitafanyika kupunguza uhamishaji wa fedha katika mafungu ya bajeti ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa mipango iliyopangwa.

Amesema Serikali itafanya maboresho katika mifumo ya usimamizi wa mapato, misaada na mikopo kwa lengo la kuchangia Sh55.2 trilioni katika Mfuko Mkuu wa Hazina, kiasi kinachowakilisha asilimia 88.6 ya makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya jumla ya Sh62.3 trilioni kwa mwaka husika.

Pia, amesema Serikali imeweka kipaumbele katika kulipa kwa wakati riba na mtaji wa deni la Serikali linalotarajiwa kuiva lenye thamani ya Sh15.1 trilioni.

Hatua hiyo inalenga kutimiza masharti ya mikataba mbalimbali ya kifedha na kuendelea kuimarisha imani ya Serikali katika masoko ya fedha ya ndani, kikanda na kimataifa.

Kuhusu madeni ya ndani ya Serikali, Balozi Omar amesema kutatengwa Sh100 bilioni kila mwezi kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi wa umma, makandarasi, wazabuni na watoa huduma.

Amesema lengo ni kupunguza malimbikizo ya madeni na kuimarisha mzunguko wa fedha katika shughuli za kiuchumi.

Aidha, Balozi Omar amesema Serikali inapanga kuboresha mfumo wa ugawaji wa rasilimali za fedha kwa kuzingatia matokeo ya tafiti za kitaalamu ili kuondoa urudufu wa matumizi na kuhakikisha uwiano mzuri wa mgawanyo wa fedha kati ya Serikali Kuu na mamlaka za Serikali za mitaa pamoja na halmashauri zenyewe.

Katika hatua nyingine, amesema tathmini ya mfumo wa usimamizi wa bajeti unaozingatia program, itaendelea kufanyika ili kusaidia kufanya uamuzi kuhusu maboresho ya usimamizi wa mipango na bajeti ya Serikali.

 Pia, amesema uwezo wa watumishi wa umma utaendelea kuimarishwa katika maeneo ya mazingira, masuala ya kijamii, utawala bora na matumizi ya teknolojia za Akili Unde (AI).

Waziri amesema pamoja na mipango hiyo, Serikali inatambua uwepo wa vihatarishi vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2026/27.

Hata hivyo, amesema wizara itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na vihatarishi hivyo ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Akiangazia hali ya uchumi, Balozi Omar amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuonesha mwenendo mzuri wa ukuaji, uliokua kwa wastani wa asilimia 5.9 mwaka 2025 ikilinganishwa na asilimia 5.5 mwaka 2024. Amesema mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi, kuboreshwa kwa miundombinu, ukuaji wa shughuli za kilimo, uchimbaji wa madini, ujenzi pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeeleza kuwa, kuna maeneo manne muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele ili kurahisisha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2026/27.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, mwenyekiti wake, Mashimba Ndaki amesema Hazina inapaswa kuandaa miongozo ya kina ya kufuatilia mtiririko wa mitaji na kuweka mifumo ya kutoa tahadhari mapema kuhusu vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika sekta ya fedha.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha mikopo inayochukuliwa na Serikali inaelekezwa katika miradi yenye tija ili kuepuka kuongeza mzigo wa deni usio na manufaa ya kiuchumi.

Aidha, ameshauri kuimarishwa kwa mifumo ya kifedha ili sekta binafsi ya ndani iweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa mitaji ya nje.

Kamati hiyo pia imependekeza kuongezwa kwa upatikanaji wa mikopo nafuu na kuendelezwa kwa masoko ya mitaji ya ndani ili kuvutia uwekezaji zaidi na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika uchumi wa Taifa.

Wakati huohuo, mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (CCM), amependekeza kutungwa kwa sheria kali zaidi dhidi ya wezi wa mali za umma na wala rushwa.

Amesema vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma vinaendelea kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa na kuwaumiza wananchi wa kawaida.

Waitara amesema hakuna fedha zinazotengwa kwa ajili ya rushwa au matumizi yasiyo na tija, hivyo wahusika wa ubadhirifu wanapaswa kuwajibishwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *