
Tanga. Ndoto ya muda mrefu ya kuhakikisha watumishi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga wanapata makazi ya uhakika na kuondokana na mzigo wa gharama za pango, imeanza kuchukua sura.
Hiyo ni baada ya kukabidhiwa hundi ya Sh500 milioni kwa ajili ya kuharakisha ujenzi wa nyumba za watumishi katika wilaya zote za mkoa huo.
Mradi huo unalenga kujenga nyumba 36 katika wilaya tisa za CCM Mkoa wa Tanga, kila wilaya itajengewa nyumba nne zitakazotumika na Katibu wa chama pamoja na viongozi wa jumuiya zake.
Kukamilika kwa nyumba hizo kunatarajiwa kuondoa utegemezi wa upangishaji wa nyumba na kufanya CCM kuokoa zaidi ya Sh90 milioni ambazo kwa sasa hutumika kila mwaka kulipia pango.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya hundi hiyo leo Jumatano Juni 3, 2026, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdurahman amesema mradi huo utakuwa mkombozi mkubwa wa kifedha kwa chama na kwamba, fedha zilizokuwa zikitumika kulipia pango sasa zitaelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.
“Kabla ya kuanza mradi huu, baadhi ya watumishi walikuwa wakilipa hadi Sh200,000 kwa mwezi kwa ajili ya pango. Ukijumlisha wilaya zote, chama kilikuwa kinatumia fedha nyingi sana kila mwaka. Kukamilika kwa nyumba hizi kutatupa nafasi ya kuokoa zaidi ya Sh90 milioni kwa mwaka na kuelekeza fedha hizo katika shughuli nyingine za maendeleo ya chama,” amesema Rajab.
Amesema fedha hizo tayari zipo benki na zitaanza kutolewa kwa awamu kulingana na hatua za utekelezaji wa mradi, huku akisisitiza kwamba chama hakitavumilia ubadhirifu wa fedha hizo za maendeleo ya chama.
“Fedha hizi ni za wanachama na ni kwa ajili ya maendeleo ya chama. Wataalamu wanaendelea na tathmini katika maeneo yote ya mradi. Wale wanaofikiria kuzitumia vibaya fedha hizi waelewe wazi kuwa hatutavumilia ubadhirifu wa aina yoyote,” amesisitiza.
Katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa amempongeza Rajab pamoja na timu yake kwa hatua kubwa waliyoifikia katika kuimarisha miundombinu ya chama mkoani Tanga, akisema mkoa huo umeanza kuwa mfano wa kuigwa ndani ya CCM.
“Nimefurahishwa na kasi ya maendeleo ninayoiona Tanga. Uongozi wa Mkoa umeonesha kwamba ukiwa na maono na usimamizi mzuri unaweza kubadilisha taswira ya chama. Miradi hii ni mfano mzuri kwa mikoa mingine kujifunza,” amesema Mabala.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Mkinga, Siza Mwegele amesema utekelezaji wa mradi huo ni ishara ya uongozi unaojali maslahi ya watumishi na maendeleo ya taasisi kwa ujumla.
“Kwa miaka mingi tumekuwa tukikabiliwa na changamoto za makazi. Ujenzi wa nyumba hizi ni suluhisho la kudumu ambalo litaboresha mazingira ya kazi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wanachama wetu,” amesema.
Wanachama wa CCM kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Tanga pia wameeleza matumaini yao kuhusu mradi huo.
Mwanachama kutoka Wilaya ya Pangani, Rashed Juma amesema hatua hiyo inaonesha utekelezaji wa vitendo wa ahadi za viongozi wa chama.
Mwanachama mwingine kutoka Wilaya ya Lushoto, Rahma Abdalah amesema mradi huo utaacha alama ya kudumu katika historia ya CCM Mkoa wa Tanga kutokana na manufaa yake kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Ujenzi wa nyumba hizo ni miongoni mwa ahadi muhimu zilizotolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdurahman, wakati akiomba ridhaa ya kuongoza chama mkoani humo.