Mirerani. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza Serikali kuongeza usimamizi kwa wamiliki wa migodi na vitalu vya madini ili kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu wajibu wao wa kutoa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Kimesema lengo la kufanya la kufanya hivyo ni kutaka wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya uchimbaji wanufaike moja kwa moja.

Maelekezo hayo yametolewa leo Jumatano, Juni 3, 2026 na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi baada ya kukagua jengo la Soko Kuu la Madini ya Tanzanite na Vito (Tanzanite Exchange Centre) lililojengwa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, kwa gharama ya zaidi ya Sh5.4 bilioni.

Kihongosi amesema CCM imefurahishwa na hatua za Serikali za kuimarisha usimamizi wa fedha za CSR, lakini kuna haja ya kuongeza ufuatiliaji ili kuhakikisha michango hiyo inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Tunaiomba Serikali kuendelea kuimarisha usimamizi wa wamiliki wa migodi na vitalu vya madini ili wananchi waone na kufurahia manufaa ya uwepo wa rasilimali hizi katika maeneo yao,” amesema.

Ameongeza kuwa fedha za CSR zimechangia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa zahanati, wadi za mama na mtoto na miundombinu ya huduma za jamii. Akizungumzia soko hilo, Kihongosi amesema ni jitihada za Serikali kuongeza thamani ya madini, kuimarisha biashara rasmi na kuongeza mapato ya Taifa.
“Soko hili linakusanya wadau wote wa sekta ya madini katika eneo moja, kuongeza uwazi, ushindani wa bei na upatikanaji wa masoko ya uhakika,” amesema.

Ofisa Madini Mkazi wa Mirerani, George Kaseza amesema soko hilo linalenga kufanya Tanzania kitovu cha biashara ya madini, huku minada miwili ya awali ikiuza madini yenye thamani ya zaidi ya Sh992 milioni.

Kaseza amesema hatua inayofuata ni kuanzisha minada ya kimataifa kuongeza ushindani na thamani ya madini ya Tanzania.

Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Grace Munuo amesema mradi wa soko ulitekelezwa kwa ushirikiano kati ya halmashauri na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ukiwa umekamilika kwa asilimia 100.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema Serikali itaendelea kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanashirikisha wadau wote, ikiwamo wa sekta binafsi na kampuni za madini.

Meneja wa Franone Mining and Gems Company Limited, Vituz Ndakize amesema ujenzi wa zahanati ulianza Septemba 12, 2025 na umefikia asilimia 98, ukitarajiwa kukamilika Juni, 2026, na utawanufaisha zaidi ya wananchi 16,000 wa Mirerani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *