Dar es Salaam. Hospitali ya CCBRT imezindua kampeni ya kitaifa ya kuchangisha Sh3 bilioni kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto wanaozaliwa na changamoto za kiafya, huku ikiweka wazi  kuwa, kujiondoa kwa wafadhili kumeathiri uwezo wa taasisi kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wasio na uwezo.

Mabadiliko hayo yaliyoanza Februari 2025 yameiweka CCBRT katika wakati mgumu wa kuendelea kutoa huduma za bure au za gharama nafuu kwa watoto wanaozaliwa na changamoto zinazoweza kutibika kama miguu kifundo, mdomo wazi, mtoto wa jicho wa kuzaliwa nao na mtindio wa ubongo.

Kupitia kampeni hiyo inalenga kuhamasisha Watanzania, taasisi na sekta binafsi kuchangia ili kuziba pengo lililoachwa na wafadhili pamoja na kuhakikisha huduma muhimu kwa watoto wenye uhitaji zinaendelea kutolewa bila kukatizwa.

Kampeni hiyo yenye kaulimbiu ya Simama na CCBRT, itatekelezwa kwa miezi mitatu.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo leo Jumatano, Juni 3, 2026 Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi amesema maelfu ya watoto nchini huzaliwa kila mwaka na changamoto za kiafya zinazoweza kutibika ikiwa watapata huduma kwa wakati.

Amesema watoto wengi hukosa matibabu kutokana na changamoto za kifedha zinazozikabili familia zao, hali inayowafanya kuishi na ulemavu wa kudumu, kukumbana na unyanyapaa na kunyimwa fursa za elimu na maendeleo.

“Kaulimbiu ya Simama na CCBRT, si ujumbe tu, bali ni wito wa mshikamano, huruma na uwajibikaji wa pamoja ili kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa na changamoto ya kiafya inayoweza kutibika anapata huduma bora za afya na nafasi ya kuwa na maisha yenye heshima,” amesema.

Msangi amesema CCBRT imekuwa ikitoa huduma za afya na utengamao kwa zaidi ya miaka 30, huku ikiwalenga zaidi watu maskini na walio katika mazingira magumu.

Amesema kwa sasa inakadiriwa kuwa watu milioni 4.2 nchini wanaishi na aina mbalimbali za ulemavu, hali inayohitaji jitihada za pamoja kutoka kwa Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wananchi kwa jumla.

Msangi amesema fedha zitakazopatikana kupitia kampeni hiyo, zitatumika katika maeneo matatu makuu ambayo ni utambuzi wa mapema wa watoto wenye changamoto hizo na kuwaunganisha na huduma za kibingwa, kuelimisha jamii ili kuondoa imani potofu kuhusu ulemavu na kugharamia matibabu jumuishi ikiwamo upasuaji, tiba ya viungo, huduma za urekebishaji pamoja na vifaa saidizi.

Amesema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha changamoto za kifedha hazimzuii mtoto kupata matibabu anayostahili.

“Tunataka kuona watoto wanatembea, wanaona, wanajifunza na kushiriki kikamilifu katika jamii. Tunataka kurejesha matumaini kwa familia ambazo zimekuwa zikiamini hakuna suluhisho kwa changamoto zinazowakabili watoto wao,” amesema.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Cyprian Ntomoka amesema hospitali hiyo imefikia hatua ya kuomba msaada wa wananchi baada ya baadhi ya wafadhili waliokuwa wakigharamia matibabu ya wagonjwa wasio na uwezo kuelekeza ufadhili wao katika maeneo mengine.

Amesema mabadiliko hayo yamesababisha kupungua kwa fedha zilizokuwa zikitumika kuwasaidia watoto na wagonjwa wengine wenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya.

“itakuwa ni bahati mbaya sana kama uwekezaji mkubwa ambao umefanywa kwa miaka mingi na wafadhili wetu utaachwa upotee kwa sababu tu, vipaumbele vyao vimebadilika. Sasa ni jukumu letu sisi kama Watanzania kusimama na CCBRT ili huduma hizi ziendelee kuwafikia wanaozihitaji,” amesema Dk Ntomoka.

Amesema hospitali hiyo haitaki kufikia hatua ya kuwaambia watoto waliokuwa wakipata matibabu bure kuwa huduma hizo hazipo tena kutokana na ukosefu wa fedha.

Dk Ntomoka ametolea mfano watoto wenye mtindio wa ubongo ambao hupata nafuu kupitia tiba ya viungo na mazoezi maalumu, yanayowasaidia kupunguza kiwango cha utegemezi kwa wazazi wao na kushiriki masomo na shughuli nyingine za kijamii.

Aidha, amesema baadhi ya watoto wenye miguu kifundo au changamoto nyingine za kuzaliwa nazo wanaweza kuishi maisha ya kawaida kabisa ikiwa watapata matibabu kwa wakati.

“Tunawaomba Watanzania wachangie kwa uwezo wao. Hatuwatafuti matajiri pekee. Mtu anaweza kutoa Sh1,000, Sh2,000, Sh5,000 au zaidi kulingana na uwezo wake. Muhimu ni moyo wa kusaidia,” amesema.

Amesema Watanzania wamekuwa wakijitokeza kuchangia shughuli mbalimbali za kijamii na kifamilia, hivyo wana uwezo pia wa kusaidia watoto wenye uhitaji wa matibabu.

Mbali na kuwanufaisha watoto na familia zao, Dk Ntomoka amesema kampeni hiyo itakuwa mchango muhimu kwa uchumi wa Taifa kwa kuwa itasaidia kurejesha uwezo wa baadhi ya watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

“Tunapomsaidia mtoto kupata matibabu na kuondokana na ulemavu unaoweza kuzuilika, tunakuwa tumewekeza katika nguvu kazi ya baadaye ya nchi yetu,” amesema.

CCBRT imewataka wananchi, kampuni, taasisi za Serikali, washirika wa maendeleo na wadau wengine kuunga mkono kampeni hiyo kwa kuchangia kupitia akaunti ya benki na mifumo ya malipo ya simu ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa matibabu kutokana na umaskini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *