
Kwa zaidi ya miaka 200, baiskeli imekuwa njia nafuu, ya kuaminika na rafiki kwa mazingira ya usafiri, ikisaidia mamilioni ya watu kusafiri, kufanya mazoezi na kuunganishwa na jamii zao.
Siku hii ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kuangazia mchango wa kipekee wa baiskeli katika maendeleo endelevu, uboreshaji wa afya na ujumuishaji wa kijamii.
Baiskeli ni njia muhimu ya kuboresha afya
Wataalamu wa afya wanasema kuendesha baiskeli ni moja ya njia rahisi zaidi za kuendelea kuwa na mazoezi ya mwili. Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO), kufanya shughuli za mwili za kiwango cha wastani kama vile kuendesha baiskeli kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari na baadhi ya saratani.
Kuendesha baiskeli pia kunasaidia afya ya akili kwa kupunguza msongo wa mawazo na kuboresha ustawi wa mwili kwa ujumla.
WHO inasisitiza kuwa hata kiwango kidogo cha shughuli za mwili ni bora kuliko kutofanya kabisa, jambo linalofanya baiskeli kuwa chaguo linalofaa kwa watu wa rika zote.
Chombo cha kukuza usawa katika jamii
Kwa watu wengi, hasa wale wanaoishi mijini na wenye kipato cha chini, baiskeli ni njia ya gharama nafuu ya usafiri.
Tofauti na magari binafsi, baiskeli haihitaji mafuta na gharama zake za matengenezo ni ndogo.
WHO inaeleza kuwa miundombinu salama ya kutembea na kuendesha baiskeli inaweza kusaidia kupunguza tofauti za kijamii kwa kuwezesha wananchi kupata ajira, shule, huduma za afya na huduma nyingine muhimu.
Hivyo, matumizi ya baiskeli hayachangii tu afya bora bali pia huongeza ujumuishaji wa kijamii na kiuchumi.
Mchango katika miji safi na mazingira bora
Kadiri miji inavyoendelea kukua, Umoja wa Mataifa unasema baiskeli imeonekana kuwa sehemu muhimu ya suluhisho la kupunguza msongamano wa magari, uchafuzi wa hewa na uzalishaji wa gesi chafuzi zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.
Baiskeli haitoi hewa chafu wakati wa matumizi na hivyo kusaidia kuboresha ubora wa hewa na kufanya miji kuwa salama na yenye afya zaidi kwa wakazi wake.
Janga la coronavirus“>COVID-19 pia lilisababisha miji mingi duniani kutathmini upya mifumo yake ya usafiri na kuwekeza zaidi katika njia za baiskeli na usafiri endelevu.
Kusaidia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu
Maadhimisho ya Siku ya Baiskeli Duniani pia yanaangazia nafasi ya baiskeli katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Mifumo ya usafiri inayohamasisha matumizi ya baiskeli inaweza kuchochea ukuaji wa uchumi, kupunguza pengo la usawa na kuimarisha mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Kutambua mchango huo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Machi 2022 lilipitisha azimio linalohimiza kuingizwa kwa matumizi ya baiskeli katika mifumo ya usafiri wa umma kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Azimio hilo lilisisitiza kuwa baiskeli ni nyenzo muhimu ya usafiri endelevu na ina mchango chanya katika matumizi na uzalishaji endelevu pamoja na juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kuimarisha mshikamano wa jamii
Mbali na kuwa njia ya usafiri na mazoezi, baiskeli inaweza kusaidia kuimarisha mahusiano ya kijamii na ushiriki wa wananchi katika shughuli za jamii.
Umoja wa Mataifa unahimiza serikali, mashirika na jamii kuandaa matembezi na safari za baiskeli katika ngazi za kitaifa na za mitaa ili kuimarisha afya ya mwili na akili.
Shughuli hizo pia zinaweza kukuza mnepo, kuelewana, kuheshimiana na ujumuishaji wa kijamii, hususan kwa watoto na vijana.
Ni zaidi ya chombo cha usafiri
Siku ya Baiskeli Duniani ni ukumbusho kwamba baiskeli ni zaidi ya chombo cha usafiri. Ni nyenzo inayochangia afya bora, mazingira safi, usawa wa kijamii na maendeleo endelevu.
Wakati dunia ikiadhimisha siku hii, ujumbe unabaki kuwa wazi, kuwekeza katika matumizi ya baiskeli ni kuwekeza katika watu wenye afya bora, jamii imara na mustakabali endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.