
Tangu mwanzo wa mwaka huu, OHCHR imesema mashambulizi yasiyopungua 12 yameripotiwa kuua karibu raia 53, wakiwemo maafisa 35 wa polisi, wavulana watano na mwanamke mmoja.
Mashambulizi manne kati ya hayo yalitokea mwezi Mei pekee, na kusababisha vifo vya maafisa 12 wa polisi.
Ofisi hiyo ya haki za binadamu imekumbusha kuwa mashambulizi yanayowalenga polisi kwa sababu tu ya kutekeleza majukumu yao ya kawaida ya kulinda usalama na kutekeleza sheria yanaweza kuhesabiwa kuwa uhalifu wa kivita.
“Miezi karibu minane imepita tangu kutangazwa kwa usitishaji mapigano, lakini bado hakuna dalili ya mwisho wa mauaji, machafuko na mateso,” amesema mwakilishi wa OHCHR katika eneo linalokaliwa kimabavu la Palestina, Ajith Sunghay.
Polisi wauawa wakitekeleza majukumu yao
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mashambulizi hayo yamekuwa yakifanyika wakati polisi wakitekeleza majukumu ya kawaida kama kudhibiti msongamano wa magari na kufanya doria katika mitaa na masoko.
Mashambulizi mengi pia yamelenga maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu, jambo linaloonesha kutokujali maisha ya raia, wakiwemo wakimbizi wa ndani, watoto na hata watu waliokuwa wamezuiliwa amesema Sunghay.
Tukio la hivi karibuni lilitokea Mei 23, wakati shambulio la Israel lilipolenga kituo cha ukaguzi cha polisi katika eneo la Al Tawam mjini Gaza na kuua maafisa watano wa polisi pamoja na watu wengine wawili, akiwemo mvulana mmoja.
Mapema Aprili 24, ndege isiyo na rubani ya Israel ilishambulia gari la polisi lililokuwa likifanya operesheni ya kutekeleza sheria katika eneo la Beer 19 ndani ya kambi ya Al Mawasi magharibi mwa Khan Younis, na kusababisha vifo vya maafisa wanne wa polisi pamoja na wanaume watatu na mvulana wa miaka tisa waliokuwa kwenye mahema jirani.
Shambulio hilo lilitokea wakati wa sala ya magharibi, ambapo Wapalestina wengi walikuwa wakielekea msikitini.
UN yaonya kuhusu kuvunjwa kwa taasisi za utawala wa umma
Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa hali hiyo inazua wasiwasi kwamba vikosi vya Israel havitofautishi kati ya polisi na wapiganaji wa makundi yenye silaha.
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu, polisi ni raia wanaostahili kulindwa dhidi ya mashambulizi isipokuwa wanaposhiriki moja kwa moja katika mapigano.
OHCHR imesisitiza kuwa mashambulizi hayo ni sehemu ya mwenendo mpana wa kushindwa kuchukua tahadhari za kutosha kulinda raia na miundombinu ya kiraia wakati wa operesheni za kijeshi Gaza.
“Israel ina wajibu wa kuhakikisha utulivu wa umma na usalama wa Wapalestina. Badala yake, kulengwa na kuvunjwa kwa taasisi za utawala wa umma kumeitumbukiza Gaza katika machafuko yenye athari mbaya kwa raia,” amesema Bwana. Sunghay.