
Dar es Salaam. Akiwa na umri wa miaka 89, rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, bado anaonekana mwenye nguvu, mchangamfu na mwenye uwezo wa kushiriki shughuli mbalimbali kama ilivyokuwa miaka mingi iliyopita. Siri ya afya yake amesema, si uchawi wala bahati, bali ni nidhamu ya maisha aliyoiweka kwa zaidi ya miongo minne tangu alipogundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari.
Katika ukumbi wa maktaba yake ya urais uliopo Abeokuta, Jimbo la Ogun nchini Nigeria, Obasanjo alisimama mbele ya wageni na kutoa simulizi la maisha yake jambo lililowavutia wengi.
Alizungumza kwa utulivu, lakini maneno yake yalibeba ujumbe mzito kuhusu umuhimu wa kujali afya.
Obasanjo alitoa kauli hiyo Jumapili Mei 31, 2026 wakati wa uzinduzi wa safari maalumu ijulikanayo kama “Lagos to the World”, inayolenga kuhamasisha jamii kuhusu saratani, umuhimu wa uchunguzi wa mapema na kuimarisha mshikamano wa Waafrika.
Alikumbuka siku alipogundulika kuwa na kisukari zaidi ya miaka 40 iliyopita. Kwa wengi, taarifa kama hiyo huja na hofu na wasiwasi mkubwa, lakini kwake ilikuwa mwanzo wa safari ya kujifunza namna ya kuishi kwa nidhamu ili kuudhibiti ugonjwa huo.
“Nina ugonjwa ambao hadi leo haujapatiwa tiba ya kuponya kabisa, nao ni kisukari. Niligundulika nao zaidi ya miaka 40 iliyopita na bado ninaendelea kuudhibiti,” alisema huku akitabasamu.
Kwa Obasanjo, siri kubwa imekuwa kutokubali ugonjwa utawale maisha yake. Badala yake, aliamua kubadili mtindo wa maisha na kuufuata kwa umakini mkubwa. Miongoni mwa mambo aliyoyapa kipaumbele ni mazoezi ya mwili.
Alieleza kuwa hadi leo bado anacheza mchezo wa squash mara tatu kwa wiki kila anapokuwa nyumbani. Jumatatu, Jumatano na Ijumaa ni siku ambazo huzitenga kwa ajili ya mazoezi hayo, jambo analosema limemsaidia kuendelea kuwa na afya njema licha ya umri wake mkubwa na kuugua kisukari.
Lakini mazoezi pekee hayatoshi. Obasanjo alisema amekuwa mwangalifu sana kuhusu chakula anachokula.
“Lishe inaweza kuwa ya kuvutia na yenye kufurahisha, lakini ukila vibaya madhara yake yanaweza kuwa makubwa,” alisema, akisisitiza kuwa watu wengi hujikuta wakiharibu afya zao kutokana na uchaguzi mbaya wa chakula.
Mbali na kula vizuri na kufanya mazoezi, kiongozi huyo wa zamani alisema amekuwa akihakikisha anapata mapumziko ya kutosha. Kwa maoni yake, mwili hauwezi kufanya kazi vizuri bila kupumzika.
Kanuni hizo zote amezipa jina la “DREMS”, mfumo wa maisha unaojumuisha lishe bora, mapumziko, mazoezi, uchunguzi wa afya wa mara kwa mara na kufuata matibabu yanayoshauriwa na wataalamu wa afya.
Obasanjo alionya kuwa watu wengi husubiri mpaka waumwe ndipo waende hospitalini, jambo ambalo mara nyingi huchelewesha ugunduzi wa magonjwa na kupunguza nafasi ya kupata matibabu kwa wakati.
“Kufanya vipimo vya afya mara kwa mara ni muhimu sana. Magonjwa mengi yanaweza kudhibitiwa vizuri yakigunduliwa mapema,” alisema.
Kwa Obasanjo, ujumbe wake ni rahisi lakini wenye nguvu: ugonjwa si mwisho wa maisha. Kwa nidhamu, lishe bora, mazoezi, mapumziko na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, mtu anaweza kuendelea kuishi maisha yenye afya na tija kwa muda mrefu.
Obasanja pia alitumia wasaa huo kumpongeza mfanyabiashara na mpenzi wa magari aina ya BMW, Erik Nwagwu, kwa kuanzisha kampeni ya uhamasishaji wa saratani kufuatia vifo vya mama na dada yake vilivyosababishwa na ugonjwa huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Nwagwu alisema safari ya “Lagos to the World” itafanyika kwa hatua kadhaa kabla ya kuzunguka dunia nzima mwaka ujao. Alieleza kuwa awamu ya kwanza itahusisha kusafiri hadi Accra nchini Ghana na kurejea Nigeria, huku awamu zinazofuata zikijumuisha safari za Senegal na baadaye mabara mbalimbali duniani.
Nwagwu alisema moja ya malengo makuu ya safari hiyo ni kuongeza uelewa kuhusu saratani ya tezi dume, ambayo imeendelea kuwa miongoni mwa sababu kuu za vifo vya wanaume barani Afrika. Alisema kupitia ushirikiano na taasisi za afya, kampeni hiyo pia itatoa huduma za uchunguzi wa saratani bila malipo kwa wananchi katika maeneo mbalimbali itakayopita.
Mbali na masuala ya afya, Nwagwu alisema safari hiyo inalenga kuonesha taswira chanya ya Nigeria na kuhamasisha ushirikiano wa Waafrika katika kutatua changamoto zinazolikabili bara hilo.