Shirikisho la Soka la Norway (NFF) lilisema jana Jumanne kwamba limeiomba kamati ya maadili ya FIFA kuchunguza tuzo ya amani iliyotolewa na baraza linalosimamia soka duniani kwa Rais wa Marekani, Donald Trump.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino, alimkabidhi Trump tuzo yake ya kwanza ya amani wakati wa droo ya Kombe la Dunia 2026, Desemba 6 mwaka jana.

Baadaye mwezi huo, kundi la kutetea haki za binadamu FairSqaure liliwasilisha malalamiko kwa kamati ya maadili ya FIFA, likisema kwamba Infantino amekiuka wajibu wake wa kutoegemea upande wowote kwa kumuunga mkono Donald Trump.

FIFA haijawahi kutoa maelezo ya utaratibu wa kutolewa tuzo hiyo ya amani, ambayo ilikuja wakati Trump na utawala wake walikuwa wakishinikiza mara kwa mara kwamba apewe Tuzo ya Amani ya Nobel.

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino ameonyesha waziwazi uhusiano wa karibu na Trump kuelekea Kombe la Dunia la Juni 11 hadi Julai 19 nchini Marekani, Canada na Mexico.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanasema kwamba hatua ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ya kumpa Tuzo ya Amani Rais Donald Trump wa Marekani ndio habari ya kipuuzi zaidi ambayo wamewahi kusikia maishani mwao.

Wanaharakati wa kimataifa wametilia shaka uamuzi wa FIFA wa kumpa Trump Tuzo ya Amani na kuudhihaki kwa kuchapisha picha na michoro ya katuni.

Wakizungumzia jinsi Rais huyo wa Marekani alivyotuma silaha zinazotumiwa na Israel katika mauaji ya kimbari ya Wapaletina wa Ukanda wa Gaza, kutochukua kwake hatua za kivitendo za kuzuia vita vya Gaza kwa wakati mwafaka na mienendo yake mingine ya kivita dhidi ya nchi nyingine kama Venezuela, Iran na kadhalika, wadau wa mitandao ya kijamii wameitaja hatua ya FIFA kuwa ni mchezo wa kisiasa usiostahili heshima ya shirika la kimataifa.

Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, baada ya kusababisha hasara za kiuchumi na kutia doa hadhi ya kijeshi na kisiasa ya Marekani sasa vimeweka kivuli kizito juu ya kinachoitwa tuzo ya amani ya FIFA kwa rais Donald Trump.

Baada ya kupokea tuzo hiyo ya kinachoitwa amani, Trump alishambulia nchi mbili—Venezuela na Iran—jambo ambalo limezua maswali mengi juu ya uhalali wa FIFA katika kutoa tuzo hiyo.

Kabla ya hapo, wanachama wengi kati ya 212 wa FIFA walikuwa wamepinga utoaji wa tuzo hiyo ya kubuniwa eti ya amani ambayo Infantino alimkabidhi rafiki yake wa karibu, Donald Trump.

Wataalamu wengi wa soka wanaamini kuwa tuzo hiyo haina hadhi yoyote kwa sababu haina vigezo vya wazi vya kumpata mshindi, na inatolewa kwa upendeleo na matakwa ya rais wa FIFA.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *