Dar es Salaam. Wakati Kenya ikiendelea kuomboleza vifo vya wanafunzi 16 waliopoteza maisha katika ajali ya moto iliyotokea katika Shule ya Wasichana ya Utumishi Academy, Gilgil, uchunguzi unaoendelea umeanza kufichua mazingira yaliyosababisha kutokea kwa mkasa huo.

Moto huo uliozuka usiku wa kuamkia Mei 28, 2026, katika bweni la shule hiyo, umetajwa kuwa miongoni mwa majanga mabaya zaidi kuwahi kutokea katika taasisi za elimu nchini Kenya katika miaka ya karibuni.

Tovuti ya Tuko Kenya imenukuliwa ikieleza kuwa taarifa za uchunguzi zinaonesha wanafunzi saba wanaoshikiliwa na polisi wamehusishwa moja kwa moja na tukio hilo baada ya kunaswa na kamera za usalama (CCTV) wakielekea katika bweni lililoungua muda mfupi kabla ya moto kuzuka.

Wapelelezi kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Mauaji na Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamesema uchambuzi wa picha za CCTV pamoja na ushahidi mwingine wa kisayansi, umewezesha kubaini baadhi ya washukiwa wanaodaiwa kuhusika katika kupanga na kutekeleza tukio hilo.

Katika maelezo yao kwa wachunguzi, wanafunzi hao walidai kuchochewa na sababu mbalimbali kuchukua uamuzi huo.

Miongoni mwa sababu zilizotajwa ni mabadiliko ya ratiba ya mitihani ya shule. Badala ya kuanza Juni 16 kama ilivyokuwa na kurudishwa nyuma hadi Juni 2,2026 jambo ambalo baadhi ya wanafunzi waliona halikuwapa muda wa kutosha wa kujiandaa.

Sababu nyingine iliyotajwa ni uamuzi wa shule kuwatoza wanafunzi fedha za kushiriki tamasha la kitamaduni lililokuwa linatarajiwa kufanyika shuleni hapo.

Kwa mujibu wa maelezo yao, hatua hiyo ilizua malalamiko miongoni mwa baadhi ya wanafunzi na kuongeza hali ya kutoridhika dhidi ya uongozi wa shule.

Aidha, uchunguzi unaonyesha kuwa baadhi ya wanafunzi walishawishiwa na matukio ya mgomo yaliyotokea katika shule jirani ya wavulana siku chache kabla ya mkasa huo. Wachunguzi wanaamini mazingira hayo huenda yalichangia kuwapa baadhi yao ujasiri wa kutekeleza mpango huo.

Ripoti za uchunguzi zinaonyesha kuwa mpango wa kuchoma bweni hilo ulipangwa saa tatu usiku na kutekelezwa takribani saa tatu baadaye, wakati wanafunzi wengi walipokuwa wamelala. Kamera za usalama zimewanasa  washukiwa wakifika katika eneo la bweni muda mfupi baada ya saa sita usiku kabla ya moto kuzuka.

Hata hivyo, wachunguzi wanaamini huenda washukiwa hao hawakuwa peke yao katika utekelezaji wa mpango huo. Miongoni mwa maswali yanayoendelea kuchunguzwa ni namna mafuta ya taa pamoja na vifaa vya kuwashia moto vilivyopatikana ndani ya shule yenye taratibu za usalama.

Kutokana na hali hiyo, polisi wanachunguza uwezekano wa kuwapo kwa watu kutoka nje ya shule waliowasaidia vifaa hivyo au kushiriki katika upangaji wa tukio hilo.

Wakati huohuo, maswali yameibuka kuhusu hatua za tahadhari zilizochukuliwa kabla ya mkasa huo. Taarifa za uchunguzi zinaonyesha kuwa walimu wawili walikuwa wamepewa taarifa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa tukio la uchomaji moto, lakini hawakuchukua hatua zinazodaiwa kuwa muhimu kuzuia hatari hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Elimu wa Kenya, Julius Ogamba, ameagiza Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC), kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya walimu hao kwa madai ya uzembe katika kutekeleza wajibu wao wa kulinda usalama wa wanafunzi.

Aidha, mkuu wa shule hiyo anatarajiwa kuwajibishwa kutokana na madai ya kutotekeleza kikamilifu baadhi ya masharti ya usalama yaliyowekwa kwa taasisi za elimu nchini humo.

Taarifa za kitabibu zinaonyesha kuwa wanafunzi 10 walifariki dunia kutokana na kuvuta moshi mwingi uliotokana na moto huo, huku miili ya wanafunzi sita ikiteketea kiasi cha kufanya utambuzi wake kuwa mgumu.

Wataalamu wa uchunguzi wa maiti wameanza kutumia vipimo vya vinasaba (DNA) kusaidia kutambua baadhi ya miili hiyo kabla ya kukabidhiwa kwa familia zao kwa ajili ya maziko.

Juni 2, 2026, washukiwa tisa walifikishwa mbele ya Mahakama ya Naivasha na upande wa mashtaka uliomba ruhusa ya kuwashikilia kwa siku 30 zaidi ili kukamilisha uchunguzi.

Waendesha mashtaka walidai kuwa bado kuna mashahidi muhimu wa kuhojiwa pamoja na ushahidi wa kisayansi unaohitaji kukamilishwa. Hata hivyo, mawakili wa utetezi walipinga ombi hilo wakisema sababu zilizowasilishwa hazitoshi kuendelea kuwashikilia washukiwa kwa muda mrefu.

Redio Capital ya nchini humo imeeleza kuwa Mahakama iliahirisha uamuzi wa kesi hiyo hadi leo Jumatano Juni 3, 2026 ili kuamua iwapo washukiwa hao wataendelea kuzuiliwa au wataachiwa kwa dhamana.

Kadri uchunguzi unavyoendelea, mkasa huo unaibua mjadala mpana nchini Kenya kuhusu usalama wa mabweni, mifumo ya usimamizi wa wanafunzi na namna ya kushughulikia migogoro ya shule kabla haijageuka kuwa majanga yanayopoteza maisha.

Kwa familia 16 zilizopoteza watoto wao, matokeo ya uchunguzi huo yanatarajiwa kutoa mwanga kuhusu kilichotokea usiku wa tukio hilo ambalo limeacha majonzi makubwa nchini Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *