Dar es Salaam. Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (Kakama) imeeleza mkakati wake wa kukuza Kiswahili kwa nchi wanachama na duniani kupitia Kongamano la 3 la Kimataifa la Kiswahili pamoja na maadhimisho ya tano ya Siku ya Kiswahili Duniani (Masikidu) ambayo yatafanyika Julai 5 hadi 7 Julai 2026 jijini Bujumbura, Burundi, huku ujumbe wa maadhimisho hayo ukilenga mjadala wa nafasi ya Kiswahili katika ulimwengu wa teknolojia na masuala ya akiliunde.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Juni 3, 2026, Katibu Mtendaji wa Kakama, Dk Caroline Asiimwe amesema katika zama za mageuzi ya kidijiti, kuna umuhimu wa kuingiza teknolojia ya Akiliunde katika sera za lugha na biashara ili kuimarisha matumizi ya Kiswahili kupitia mifumo ya tafsiri za papo kwa papo, huduma za kidijiti za biashara na majukwaa ya mawasiliano ya kikanda.

“Hii itaongeza ushiriki wa wafanyabiashara katika soko la pamoja na kuimarisha ushindani wa kikanda. Kiswahili kinapaswa kupewa kipaumbele katika sera za biashara, uwekezaji na uchumi wa kidijiti wa Afrika Mashariki,” amesema.

Akizungumzia mustakabali wa Kiswahili katika enzi ya teknolojia, Dk Asiimwe amesema maendeleo ya Akiliunde, tafsiri za mashine, mifumo ya utambuzi wa sauti na majukwaa ya kidijiti yanabadilisha namna watu wanavyowasiliana na kujifunza.

Hata hivyo, amesema kuna haja ya kuhakikisha Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika zinapata nafasi stahiki katika teknolojia hizo.

“Tunataka kuona mwanafunzi akijifunza kupitia programu za Kiswahili zinazotumia Akiliunde, mkulima akipata taarifa za masoko kwa Kiswahili kupitia simu yake ya mkononi na mjasiriamali akitumia teknolojia za lugha kufikia masoko mapya. Tukikuza Kiswahili leo, tunafungua fursa za kesho,” amesema.

Dk Asiimwe ambaye ni mwanataaluma wa Kiswahili, amesema Kiswahili kinaendelea kuwa daraja muhimu katika kukuza biashara ya kikanda kwa kuondoa vikwazo vya mawasiliano vinavyoweza kuathiri shughuli za kiuchumi.

Amesema wafanyabiashara kutoka majijini kama Arusha, Mombasa, Bujumbura, Kigali na Goma hunufaika kwa kutumia Kiswahili kwani hupunguza gharama za tafsiri, kuokoa muda na kuongeza ufanisi wa shughuli zao za biashara.

Aidha, amesema usanifishaji wa istilahi za biashara, usafirishaji na forodha kwa Kiswahili unawezesha mawasiliano ya moja kwa moja katika mipaka ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na hivyo kupunguza ucheleweshaji wa mizigo pamoja na gharama za miamala ya biashara.

Ameongeza kuwa matukio hayo yataweka mkazo maalumu kwa vijana kupitia warsha na maonyesho ya kiteknolojia yatakayowajengea uwezo wa kukitumia Kiswahili kama fursa ya ajira, ubunifu na ushindani wa kimataifa.

Amesisitiza dhana ya kuwajumuisha vijana katika juhudi za kukuza Kiswahili ni njia ya kulinda urithi wa lugha hiyo, huku ikiandaliwa kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo katika siku zijazo.

Dk Asiimwe ametoa wito kwa wananchi, wanazuoni, watafiti, wabunifu wa teknolojia, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kiswahili na Maadhimisho ya Tano ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani.

Amesema matukio hayo yatatoa fursa ya kujadili mustakabali wa Kiswahili katika ulimwengu wa wingilugha na Akiliunde, kujenga ushirikiano mpya na kuibua suluhisho za pamoja kwa maendeleo ya lugha za Afrika Mashariki.

“Mti mmoja haujengi msitu. Kwa ushirikiano wetu, Kiswahili kitaendelea kuwa daraja la mawasiliano, chombo cha utangamano wa kikanda na nguzo ya maendeleo endelevu kwa wananchi wote wa Afrika Mashariki,” amesema.

Sambamba na hilo, nchi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekuwa katika kampeni mbalimbali kuhimiza ushiriki wa wananchi wake katika maadhimisho hayo yatakatofanyika Bujumbura.

Aidha Wizara ya Habari, Utamaduni na Utalii nchini Somalia, kwa ushirikiano na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki imezindua rasmi kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji inayowaalika wataalamu wa teknolojia, wasomi na watafiti kuwasilisha muhtasari wa tafiti zao kwa ajili ya Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kiswahili linalotarajiwa kufanyika Bujumbura.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kakama maadhimisho hayo yatatoa jukwaa kwa wanaisimu, wataalamu wa teknolojia, watunga sera, vijana na wadau mbalimbali kujadili namna Kiswahili kinavyoweza kuendelea kukua na kushindana kimataifa katika enzi ya kidijiti.

Matukio hayo mawili yatafanyika chini ya kaulimbiu inayosema “Kiswahili, Wingi lugha na Akiliunde”, kwa lengo la kujadili nafasi ya Kiswahili katika ulimwengu wa teknolojia, akiliunde (AI) na jamii za wingi-lugha.

Washiriki mbalimbali wanaotarajiwa kushiriki kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Somalia na Burundi ambao ndiyo wenyeji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *