Kupitia taarifa yao iliyotolewa mjini Geneva Uswisi, wataalam hao wamesema mlipuko huo, ambao umetangazwa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO) kuwa Dharura ya Afya ya Umma ya Kimataifa, umeenea zaidi ndani au karibu na maeneo ya watu wa jamii za asili, hali inayowaweka katika mazingira magumu zaidi.

Wataalamu hao wameangazia hasa jamii za watu wa asili wa Pygmy, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na kutengwa kijamii na kiuchumi.

 Wamesema maisha yao yanategemea kwa karibu ardhi zao za asili, misitu na rasilimali za mazingira kwa ajili ya kujikimu, utambulisho wao na ustawi wao. 

Hata hivyo, upatikanaji mdogo wa huduma za afya unaifanya jamii hiyo kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuathiriwa na ugonjwa huo unaosambaa wa Ebola

“Jamii hizi, ambazo maisha yao yanategemea kuhama-hama, zinategemea kwa karibu maeneo yao na rasilimali za asili kwa ajili ya kujikimu, utambulisho na ustawi wao. Aidha, upatikanaji  mdogo wa huduma za afya unawaweka katika hatari kubwa ya kuathiriwa na mlipuko huu,” wamesema wataalamu hao.

UN/Martine Perret Shughuli za mazishi ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa wa Ebola katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DR Congo (kutoka maktaba)

Changamoto zao zitambuliwe na kughulikiwa

Wataalamu hao wamekaribisha juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali za DRC na Uganda kudhibiti mlipuko huo, lakini wakatoa wito kwa mataifa mengine, jumuiya ya kimataifa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa watu wa jamii za asili wanapata huduma za afya kwa usawa na bila ubaguzi. 

Pia wametaka kuwepo kwa msaada maalum unaolenga jamii hizo ambazo tayari zimeathirika au ziko katika hatari ya kuambukizwa.

“Hatua za kukabiliana na Ebola lazima ziongozwe na viwango vya kimataifa vinavyohusu haki za watu wa jamii za asili, ikiwemo haki yao ya afya, ulinzi sawa mbele ya sheria na utambulisho wao wa kitamaduni,” wamesisitiza wataalamu hao. Wameonya kuwa mafanikio ya kudhibiti mlipuko huo yatategemea uwezo wa wadau kutambua na kujumuisha mahitaji maalum ya watu wa jamii za asili katika mikakati ya hatua.

 “Udhaifu wa kipekee wa watu wa jamii za asili katika kukabiliana na mlipuko huu lazima utambuliwe na kujumuishwa kikamilifu katika mikakati ya hatua,” wamesema, wakionya kuwa kutofanya hivyo kunaweza kuongeza pengo la usawa na kuwaacha baadhi ya watu walio katika hatari kubwa zaidi bila ulinzi wanaouhitaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *