
Dar es Salaam. Kizazi cha watoto waliozaliwa kati ya miaka ya 2010 hadi 2024 maarufu ‘Gen Alpha’, kinakuwa katika mazingira ambayo wazazi wao na hata babu zao hawakuwahi kuyashuhudia.
Hiki ni kizazi cha kwanza duniani kukulia katika mazingira ambayo akili unde (AI), simu janja, mitandao ya kijamii, michezo ya mtandaoni hadi taarifa zisizoisha kutoka pande zote za dunia zikiwa zimetawala.
Pia ni kizazi kinachokabiliwa na msukumo mkubwa wa taarifa na teknolojia tangu wakiwa wadogo.
Tafiti za hivi karibuni zinaonesha hali hiyo inawalazimu wazazi kubadilisha mbinu za malezi, kutoka kwenye udhibiti mkali wa teknolojia kwenda kwenye kuwajengea watoto uwezo wa kuitumia kwa usalama, uwajibikaji na manufaa.
Utafiti wa mapitio ya tafiti 34 uliochapishwa Mei 2026 katika jarida la Jurnal Pendidikan Tambusai ulibaini watoto wa Gen Alpha hunufaika zaidi pale ambapo wazazi na walimu wanatumia mkakati mmoja wa malezi ya kidijitali, ikiwemo kuweka sheria zinazofanana kuhusu matumizi ya teknolojia nyumbani na shuleni.
Hata hivyo, wataalamu wa maendeleo ya mtoto wanasema mazingira haya mapya yanaathiri namna watoto wanavyofikiri, kujifunza na kuwasiliana.
Hali hiyo imeibua mjadala kuhusu umuhimu wa kubadili baadhi ya mbinu za malezi ili kuendana na mahitaji ya kizazi hiki, huku ikisisitizwa wazazi wanapaswa kuangalia upya namna wanavyowalea watoto ili kuwajengea maadili, uwezo wa kufanya maamuzi na kukabiliana na changamoto za maisha.
Akizungumza na Mwananchi, Juni 2, 2026 Mtaalamu wa saikolojia na mahusiano nchini, Ramadhani Masenga amesema wazazi wengi wa sasa wamejikita zaidi katika kutimiza mahitaji ya msingi ya watoto kama ada, chakula na makazi salama, huku wakisahau jukumu la kuwaongoza kitabia na kimaadili katika mazingira ya sasa ya teknolojia.
“Wengi wanafikiri kulea ni kuhakikisha mtoto anakula, anasoma na ana mahali pa kuishi. Lakini malezi ni zaidi ya hapo. Ni kumsaidia mtoto kujua anapaswa kuwa mtu wa aina gani baada ya kukua. Usipomwongoza katika ulimwengu huu wa teknolojia, anaweza kupotea,” amesema.
Amefafanua mtoto huzaliwa bila uelewa wa kutosha kuhusu dunia inayomzunguka, hivyo wazazi wana jukumu la kumuongoza hatua kwa hatua. Alilinganisha hali hiyo na mtu aliye kwenye chumba chenye giza anayehitaji kuonyeshwa mlango wa kutoka.
Ramadhani Masenga pia amesisitiza kuwa mazingira yana mchango mkubwa katika kumjenga mtoto, hivyo wazazi wanapaswa kuwa makini katika kusimamia matumizi ya teknolojia na maudhui wanayokutana nayo watoto wao.
“Zamani mtoto alilazimika kutafuta njia za siri kuona mambo yasiyofaa. Leo kila kitu kipo mkononi kupitia simu. Hii inahitaji wazazi kuwa karibu zaidi na watoto wao,” amesema.
Katika mgawanyo wa majukumu ya malezi, Masenga amesema mama na baba kila mmoja ana nafasi muhimu. Mama mara nyingi huwa karibu zaidi na mtoto katika hatua za awali, akijenga hisia za upendo, huruma, mawasiliano na uaminifu, jambo linalomsaidia mtoto kujifunza kueleza hisia zake kwa usahihi.
Kwa upande mwingine, baba hutajwa kuwa nguzo ya uongozi ndani ya familia, akihusika zaidi na kuweka misingi ya nidhamu, maamuzi, uwajibikaji na kumjengea mtoto uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha bila kutegemea hisia pekee.
Ramadhani Masenga ameongeza kuwa jukumu la mwanaume ndani ya familia halipaswi kuishia katika kutafuta kipato pekee, bali pia kushiriki kikamilifu katika malezi na kuwa mfano wa maadili kwa watoto.
Amesema mtoto wa kiume au wa kike anapokosa uwiano huo wa malezi anaweza kukua bila kupata taswira sahihi ya majukumu ya kijamii, jambo linaloweza kuathiri mahusiano yake akiwa mtu mzima.
Kwa mujibu wake, malezi bora ya sasa yanahitaji wazazi wote wawili kushirikiana kwa karibu, kila mmoja akitimiza wajibu wake kwa uwiano unaojenga utu, nidhamu na uelewa wa kijamii kwa mtoto.
Tafiti za kitaalamu
Wataalamu wa afya ya akili ya watoto wanaeleza tabia ambazo mara nyingi hutafsiriwa kama ukaidi, uvivu au kutosikiliza zinaweza kuwa ishara za uchovu wa akili au msisimko mkubwa wa taarifa anazokutana nazo mtoto.
“Mtoto anayekataa kufanya jambo si lazima awe mkaidi. Wakati mwingine anaweza kuwa amechoka kiakili kutokana na msisimko mwingi wa mazingira yanayomzunguka,” amesema Anastasia Misirli mtaalamu wa afya ya akili za watoto kutoka Chuo Kikuu cha Turin, Italia.
Utafiti wake unaonyesha kuwa matumizi ya teknolojia yanaweza kusaidia au kuathiri mawasiliano ya watoto, kutegemea namna yanavyosimamiwa na watu wazima.
Katika dunia ya sasa, watoto hutumia muda mwingi mbele ya skrini kuliko vizazi vilivyopita. Ingawa teknolojia imeleta fursa nyingi za kujifunza, wataalamu wanaonya kuwa matumizi yasiyodhibitiwa yanaweza kuathiri usingizi, umakini na afya ya kihisia.
Mwaka 2025, mapitio ya tafiti yaliyochapishwa katika jarida la Frontiers in Psychology yalibaini kuwa matumizi makubwa ya skrini zikiwamo za simu, kompyuta, tableti au luninga kwa watoto wadogo yanaweza kuathiri maendeleo ya lugha na mawasiliano ya kijamii, hasa pale ambapo skrini zinachukua nafasi ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya mtoto na mzazi.
Watafiti hao walisisitiza kuwa licha ya maendeleo ya teknolojia, mazungumzo ya ana kwa ana, kusoma vitabu pamoja na michezo ya kijamii bado vina mchango mkubwa katika ukuaji wa ubongo wa mtoto.
Aidha, utafiti mwingine uliochapishwa mwaka 2025 katika jarida la Scientific Reports chini ya Nature Portfolio ulionyesha kuwa matumizi makubwa ya skrini yanaweza kuhusishwa na changamoto za usingizi, umakini na afya ya akili kwa watoto na vijana.
Kutokana na hali hiyo, wazazi wanashauriwa kuweka mipaka ya matumizi ya vifaa vya kidijitali, kuhimiza watoto kushiriki michezo ya nje, kufanya mazoezi ya mwili na kupata muda wa kutosha wa kupumzika.
Wataalamu pia wanasisitiza umuhimu wa kuwajengea watoto kile kinachoitwa ‘digital resilience’ uwezo wa kutumia teknolojia kwa usalama, kutambua hatari za mtandaoni na kufanya maamuzi sahihi wanapokutana na taarifa mbalimbali.
Utafiti wa mwaka 2026 kuhusu Gen Alpha unahitimisha kuwa watoto wanaofundishwa ujuzi huo wana nafasi kubwa ya kutumia teknolojia kwa manufaa kuliko wale wanaozuiwa kabisa kuitumia.
“Lengo si kuiga tu namna tulivyolelewa sisi. Dunia imebadilika, hivyo hata mahitaji ya watoto yamebadilika. Tunapaswa kuwasaidia kukua wakiwa na afya njema ya akili na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha ya sasa,” amesema Dk Tiia Tulviste.
Kadiri teknolojia inavyoendelea kubadilisha maisha ya kila siku, wataalamu wanaamini kuwa mafanikio ya malezi hayataamuliwa na ukali wa sheria za nyumbani pekee, bali pia uwezo wa wazazi kuelewa dunia ambayo watoto wao wanaishi na kukua ndani yake.