Simanjiro. Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amewaonya viongozi wa chama na Serikali kuacha kujigamba kwa madaraka na kujitumia heshima za uongozi, akisisitiza kwamba hakuna mtu mkubwa kuliko CCM.

Kihongosi ametoa onyo hilo leo Jumatano, Juni 3, 2026, wakati wa kikao cha mabalozi wa Shina namba nane, Tawi la Tunduru, kilichofanyika Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.

Akizungumza katika kikao hicho, Kihongosi amesema viongozi wanapaswa kutambua kuwa heshima na mamlaka wanayoyapata yanatokana na chama, si uwezo wao binafsi.
“Tunapokuwa viongozi lazima tutambue kwamba heshima tulizonazo leo zinatokana na CCM. Mimi mwenyewe, kama chama kingeiondoa dhamana yangu, ningekuwa raia wa kawaida,” amesema.

Amesisitiza kwamba hakuna kiongozi anayeweza kujivuna au kudharauliwa kwa sababu ya cheo chake, bali jukumu kuu ni kuwatumikia wananchi na kutekeleza majukumu waliyopewa.
“Kama ni Mwenyekiti wa mkoa, diwani, mbunge au kiongozi yeyote, chama kikiondoa dhamana hiyo, nafasi haiwezi kuendelea kuwepo. Hatupaswi kujigamba, tunapaswa kufanya kazi,” amesema kiongozi huyo.

Kihongosi pia amesisitiza kuwa CCM haitasita kuchukua hatua kwa kiongozi yeyote atakayekiuka maadili, utaratibu na misingi ya chama bila kujali nafasi yake.
“Chama kina taratibu zake na mamlaka yake. Kila anayefanya jambo lisilofaa atakumbana na vikao vya maamuzi,” amesema.

Aidha, Kihongosi ameweka mkazo kwenye umuhimu wa ushirikiano kati ya chama, Serikali na wananchi.
“Mimi ni muumini wa mshikamano na kushirikiana. Hatutamani kuona vurugu katika Wilaya hii ya Simanjiro. Tunachohitaji ni kazi, maendeleo na wananchi kunufaika na matunda ya uongozi wetu,” amesema.

Ameongeza kwamba kila kiongozi anayepewa dhamana lazima atambue kuwa anamuwakilisha Rais na kazi yake lazima iwaguse wananchi moja kwa moja.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amesema Serikali itaendelea kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanashirikisha wadau wote wa maendeleo, ikiwemo sekta binafsi na kampuni za uchimbaji madini.

“Msimamo wetu ni kwamba kila mdau atashiriki katika maendeleo ya jamii kulingana na ukubwa wa shughuli zake. Ujenzi wa zahanati hii ni mfano mzuri wa namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na Serikali kuwaletea wananchi huduma muhimu,” amesema Sendiga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *